February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

PALE UNAPOFANYA BIASHARA YA KUUZA NA KUNUNUA WATU KWA KUJUA BILA KUJUA

Denis Mpagaze

Kasi ya kuuza watu ulimwenguni ni kubwa kwa sababu ina wadau wengi. Biashara hii imekuwepo tangu enzi za Yesu na imegoma kuisha! Enzi nzile iliitwa Slave Trade, enzi hizi inaitwa Human Trafiking! Ni biashara ileile katika midundo tofauti! Zamani ilidunda kimabavu, siku hizi inadunda kilaghai. Mtoto wa maskini akikutana na mnunuzi kutoka mjini yuko tayari kuacha vyote na kuambatana naye mithili ya kuku anayejipeleka kuchingwa kwa hadaa ya punje za mahindi! Akiishafika huko ndo anaamini kumbe binadamu ni bidhaa!

Katika biashara hii kila mtu ni mshirika kwa kujua au kutokujua ingawa wengi wanakataa. Wanajua biashara hii ni ya kusafisirisha watu kutoka Somalia kwenda Afrika Kusini kwa sababu tu huwa anaona malori yaliyobeba watumwa hao yamekamatwa; wengine wanajua ni biashara inayofanyika huko Uarabuni baada ya kuona video za mabinti wakiteswa na mwingine anajua biashara hii inafanyika huko Libya baada ya kusikia Waafrika wakizamishwa Bahari ya Mediterania wakati wakijaribu kwenda kuzengea maisha Ughaibuni!  

Hakuna anayeona binti zetu wakisafirishwa kutoka vijijini kwenda mijini kufanyishwa kazi za ndani, baa, madanguro, guesthouse na mashambani kwa malipo ya kishenzi na matendo ya fedheha kama ni biashara haramu ya binadamu! Ilifikia kipindi hapa Tanzania ukitaka mabinti wazuri wa kazi za ndani agiza Iringa, ukitaka wahudumu wazuri wa baa agiza Singida na Mbulu, ukitaka vibarua wazuri wa mashambani agiza Kigoma, Ulambo wanaagiza sana bidhii hiyo kutoka Kigoma, wanaitwa wakeraji.

Kazi yako ni kuagiza watu kama unavyoagiza ng’ombe, mbuzi na mkaa kutoka mikoani! Hii ni biashara haramu inayofanyika Tanzania ingawa kati ya watu 1200 niliowauliza kuhusu kutenda dhambi ni asilimia 2 tu ndo walikubali, wengine wote walikana! Siku zote mwizi hakubali kosa.

Jamaa mmoja alitangaza kutafuta mabinti warembo kwa ajili ya kuhudumu kwenye baa yake. Mzoefu mmoja akamwambia ukitaka watu hawa nenda mikoani lakini ngoja nikupe angalizo tu, “Kama utaleta wahudumu wazuri sana jiandae kukaa nao muda mfupi manake kuna vijana watawachukua jumla kwenda kuwaoa na kazi inaishia hapohapo. Mimi nina uzoefu na hizi stress. Ukitaka wakae hakikisha uwe na wateja wanaoacha chenji, wasiwe wagumu sana utawakosa. Kazi kwako!”

Hii ni biashara ya usafirishaji haramu ingawa hakuna anayeshituka kirahisi. Hawa binadamu wanauzwa baa! Wanunuzi ni wanaume na vijana. Katika baa nyingi ukitaka kuondoka na mhudumu unamnunua kwa 10,000 kwa boss wake. Boss ameuza binadamu na wewe umenunua binadamu halafu wewe na boss wako mkiulizwa mmewahi kufanya biashara ya binadamu mtakataa. Mtasema biashara ya binadamu inafanyika Uarabuni! Hapa kuna mawili. Kujua au kutokujua.

Kuna watu wanaprojects za kuuza watu mchana kweupe. Anakwenda vijijini, anakusanya mabinti kwa kuwalaghai wazazi wao kwamba anakwenda kuwatafutia kazi kwenye hoteli za kitalii akiwafikisha mjini anawauza kwa pesa na dolali; mmoja huwa ni kati ya laki moja hadi laki mbili inategemea bargaining ya mteja! Binti aliyelaghaiwa kwenda kufanya kazi kwenye hoteli ya kitalii anaangukia kwenye kazi za ndani, full kuhenyeshwa utadhani kuna kitu alimkosea motherhouse.

Siku ya mwezi ikifika binti anaambiwa ‘nakutunzia mshahara wako as if huna akili’. Akijifanya kudai anaitwa mchawi. Madada wengi wa kazi wanaitwa wachawi kwa kudai vya kwao. Ndio maana siku hizi wananyonga watoto wenu na wengine wanawalisha chakula chenye mikojo yao. Madhara yake ni makubwa!  

Halafu wakati binti huyo yuko kwako akihenyeka, baba yake naye anakomaa mshahara umtumie yeye. Anakupiga bit hadi unatuma. Hapa baba wa binti anafanyabiashara haramu lakini ukimuuliza ataapa mbele za Mungu kwamba hajawahi kufanya biashara hiyo haramu na wala hawezi kuifanya. Atakwambia inafanyika huko Uarabuni kwa sababu tu aliona video ya binti aliyeuzwa huko ikisambaa.

Halafu baada ya kula mauzo ya mtoto wake bila huruma asubuhi anawahi misa ya kwanza na sadaka anatoa kabisa Mungu ambariki. Mungu anakubariki vipi kwa kutoa sadaka chafu! Ndo maana pamoja na kutoa kwako sadaka bado unaendelea kutembelea kucha.

Sikiliza wewe mzazi! Bila kuacha dhuluma hiyo utakuwa mtu wa kuwatangazia wapendwa wakuombee kwa majaribu unayopitia. Hukumbuki majaribu anayopitia mtoto wako huko mjini kwa sababu yako! Ujinga hauui ila unatesa sana! Baba anateseka dhambini kwa sababu ya kula vilivyotokana na mauzo ya mtoto wake! Watumishi wa Mungu chukueni hili! Linaweza  kuokoa wapendwa wenu!

Watoto wetu wamekuwa watumwa wa ngono, wanafanyishwa kazi za shuruti hadi kufa. Kuna wanaopotea baharini wakati wa safari! Kuna msako umewahi kutokea huko kwenye bahari kuu, wamiliki wa meli waliamua kuwatupa watoto wetu wote baharini ili wasikamatwe. Mtoto wako anatupwa baharini, mama hujui. Miaka nenda rudi unaishi ukimlilia mwanao kumbe aliishaliwa na mamba kitambo na kaburi lake hutoliona tena kwa sababu tu ulikubali kudanganyika!

Lakini watoto wengine wanapewa na hati za kusafiria kabisa na mamlaka husika bila kufuatilia mtoto wetu anakwenda wapi. Hii siyo sawa kabisa. Halafu wakifika huko ughaibuni wananyang’anywa hati hizo za kusafiria na kuanza maisha ya jehanamu kabla ya kufa.

Kuna Msichana alipelekwa China na mtandao wa washenzi kufanya kazi kwenye hoteli za kitalii akaishia kuburudisha wanaume wenye msongo kwenye madanguro. Msichana huyo alifanikiwa kutoroka na kurudi nyumbani ameathirika kimwili na kisaikolojia, baada ya kuwatoroka watesi wake. Binti mwingine anasema anafanya kazi ya kuburudisha wanaume wenye stress. Wajibu wake ni kuwa msafi na kupendeza. Kipato anachopewa ni kwenda kununua nguo nzuri, mafuta mazuri, perfume na saluni.

Hatima ya biashara hii haramu iko mikononi mwetu wenyewe kwa sababu wanunuzi tunawajua! Tunaishi nao. Tunakula nao. Wengine ni washikaji wetu. Inashangaza kuona mitandao hiyo ikifanya biashara hiyo kiulaini na sisi tupo! Haiwezekani. Kwanza sikilza! Hii biashara inaofanyika ndani  ya nchi huku tukiuchukulia poa ndizo cheche ziwashazo moto kuwa mkubwa na kustawisha biashara hii haramu duniani kote.

Leo hii nchi ya  Moldova ndo kinara katika uvunaji na uuzaji wa viungo vya binadamu ikifuatiwa na Uchina! Unadhani viungo hivyo vinatoka wapi kama siyo kwa hawa watoto wetu wanaosafirishwa kilaghai? Kiungo kama figo tu kinauzwa mpaka million 90 za Kitanzania. Matukio ya watu kutekwa na kuzimishwa kisha kuamka akiwa ana mshono mkubwa upande wa mbavuni ni jambo la kawaida huko Moldovo.

Unaambiwa asilimia 10% ya figo zote duniani hutokea Moldova. Maskini mmoja anasema nikiuza hizi figo zangu mbili kisha nikanunua na kuwekewa moja kuu kuu si nakuwa nimeshapata mtaji kabisa? Baada ya hapo sinywi cha pombe, coca wala nini! Nagonga maji tu kuipunguzia kazi figo yangu ya mtumba! Uongo mwanangu? Tatizo la njaa ni ile hali ya kukimbilia kichwani!

Jamani suala la usafirishaji wa binadamu tusilichukulie poa kabisa!Waliopitia hayo madhila wanakwambia baada ya kusafirishwa kuvuka mpaka wa nchi yako tu unajikuta umetekwa nyara na mtandao wa ulanguzi, huwezi kuchomoka. Mkifika huko mnapewa vibali vya kuishi kama wahamiaji haramu ili mnyonywe.

Madhara ya biashara hii ni makubwa. Yanapunguza nguvu kazi ya familia, kijiji na taifa! Lakini pia inaongeza dharau kwetu Waafrika! Kazi ya maskini sasa imebaki ni kuzaa watoto na kwenda kuwauza! Hii wiyo sifa, wala siyo utajiri. Unapeleka mwanao akatumike. Hakuumbwa kwa lengo hilo!

Nimalizie kwa simulizi hii ya kweli

Siku nyumba ya bosi wake ilipopigwa shoti Dada wa kazi alijitosa kukanyaga maji yaliyokuwa sakafuni, akapigwa shoti lakini hakusikia, alichosikia ni kilio cha mtoto wa boss ndani ya nyumba inayowaka moto! Dada akafanikiwa kumuokoa mtoto yule! Baada ya kutoka motoni na mtoto salama ndipo akagundua kuwa miguu haifanyi kazi, imeungua vibaya, akapelekwa hospitali, akalazwa miezi kadhaa, alipopata nafuu alirudishwa kijijini kwa wazazi wake, boss wake hamuhitaji tena maana hana miguu.

Binti akawapelekea wazazi wake zawadi ya kovu la miguu lilitokana na kuungua akimuokoa mtoto wa boss; Dada akaanza kuishi na kovu lisilo tazamika mara mbili; Dada hana thamani tena kwa sababu mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe! Unapata wapi nguvu huna miguu? Kwakuwa cha muhimu ilikuwa ni kuokoa mtoto basi hahitajiki tena labda hadi nyumba ikiungua tena! Binti anatunzwa na wazazi wake, amekosa hata mume wa kuoa! Wanaogopa kovu lililosababishwa na mtoto wa boss!  

Hawa watoto wanafanyiwa mambo mabaya sana. Kuna mtoto wa kihehe Arusha alichomwa mikono. Kuna mwingine alichomwa na pasi sehemu za siri maskini nadhani unakumbuka.

Kataa biashara hii kwa nguvu sanaa, halafu rusha shilingi 5000 za bando nikurushie vitabu 30!