March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

OLENGURUMWA ATAKA SHERIA ZINAZOTUNGWA ZIAKISI MAONI YA WADAU

Na Hilder Ngatunga

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),Onesmo Olengurumwa amesema mchakato wa utungaji wa sheria nchini Tanzania sio shirikishi kwa madai kuwa sheria zinazotungwa haziakisi matakwa na maoni shirikishi kutoka wadau husika.

Olengurumwa amesema hayo hii leo Mei 11, mjini Mororgoro wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari za mtandaoni yanayoendelea tangu Mei10 hadi 12.

“Tunapopima ubora wa sheria tunaanza kuangalia kwenye mchakato wa upatikanaji wake kama umekuwa shirikishi au kama umeakisi matakwa ya wadau,mnaweza mkatoa maoni lakini yasijumuishwe mwishoni”ameeleza Olengurumwa.

Aidha ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano, sheria nyingi zimekuwa zikipitishwa kwa dharura hivyo wakati mwingine kuwanyima wadau fursa ya kutoa maoni yao wakati wa mchakato wa kutungwa kwa sheria hizo.

“Zipo sheria zimetungwa kwa miaka hii sita makusudi kwa ajili ya kikundi ama watu fulani mfano kutuzuia sisi kwenda kushitaki mahakamani au kupeleka mashauri yenye maslahi ya umma mahakamani,” ameongeza Olengurumwa na kulalamikia kuwa wadau wanapotoa mapendekezo ya kuanzishwa kwa sheria mpya serikali inatumia mwanya huo kuondoa mapendekezo ya awali, akitolea mfano wa pendekezo la kuanzishwa kwa Sheria ya Huduma ya vyombo vya Habari ya mwaka 2016.

Kwa nyakati tofauti,Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania na wadau wengine wamekuwa wakipigia upatu mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazotungwa kuwa zinaminya uhuru wa kujieleza kinyume na Katiba.

“Uhuru wa kujieleza ni msingi wa kulinda na kuheshimu haki za binadamu na sheria zinazotungwa hazipaswi kuizuia haki hii na kufanya kushindwa kwa haki zingine” ameongeza Olengurumwa.