Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, ametoa wito kwa vyombo vya dola na jamii kwa ujumla, kufanya utafiti juu ya chanzo cha uibukaji makundi ya watoto wanaojihusisha na uhalifu (Panya Road).
Olengurumwa ametoa wito huo akizungumza katika mjadala wa kujadili nafasi ya vyombo vya habari kwenye kuripoti matukio ya kihalifu na haki za binadamu, ulioandaliwa na Chama cha Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) uliofanyika kwa njia ya Mtandao.
“Sasa hivi tunazungumzia Panya Road, sidhani kama kuna utafiti unaofanyika kujua tatizo la Panya Road ni nini. Lazima twende mbali tuangalie kwa nini tunakuwa na watoto wengi wanaojikusanya kuwa Panya Road, tuangalie wamekutana na nini. Vyombo vya habari viangalie kwa nini wanakuwa hivyo,” amesema Olengurumwa.
Naye Mwenyekiti wa OJADACT, Edwin Soko, amevitaka vyombo vya habari vijikite zaidi katikia kutoa taarifa zenye lengo la kuelimisha jamii kuhusu uhalifu, hususani madhara yake ili wahusika waache kutekeleza vitendo hivyo.
“Watu wanatakiwa waelewe jinsi gani uhalifu umetokea, kwa namna ipi uhalifu umetokea ili kuchukua tahadhari na wao kuwa makini ili uhalifu usitokee. Ni vyema kuripoti ili wananchi wachukue tahadhari,” amesema Soko.
Aidha amesema jamii inahitaji kufahamu kuhusu masuala ya kihalifu umefanyikaje ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya matukio hayo na pia wanataka kuona wale wanaofanya uhalifu wanachukuliwa hatua gani.
Pia amewataka waandishi wa habari kuripoti masuala ya uhalifu kwa kuzingatia weledi na mizania sawa ili kuepuka kuingilia uchunguzi pamoja na kutoa vichwa vya habari inayoweza kutafsiriwa kama wanaunga mkono matukio hayo.
Amesema OJADACT itaendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya namna ya kuripoti matukio ya uhalifu.
Kamishna wa Fedha na Lojistiki wa Jeshi la Polisi, CP Hamad Hamis Hamad, amevitaka vyombo va habari kutumia vyanzo vya Polisi katika kuripoti taarifa za kihalifu, hususan zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii, ili kudhibiti usambazaji wa taarifa za kughushi zenye kuzua taharuki kwa jamii.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa vyombo vya habari kuhamasisha Watanzania kushirikiana na Polisi katika ulinzi wao na mali zao, kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kushughulikiwa kabla uhalifu haujatokea na kuleta madhara kwa watu,” amesema CP Hamad.
Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, SACP David Misime, amevitaka vyombo vya habari visiandike habari kwa kukurupuka ili kukwepa taharuki.
“Vyombo vya habari vihakikishe taarifa inazotoa hazikuzi uhalifu zaidi, hazileti hofu kwa jamii lakini pia kuharibu ushahidi na kuwapa wahalifu sifa zaidi. Mfano kusema panya road ambao vijana wadogo wamefunga mtaa. Wanafungaje mtaa wakati wanaume wapo,” amesema SACP Misime na kuongeza:
“Tunatoa wito kwa vyombo vya habari kutoa taarifa ambazo wananchi wanazielewa bila kuathiri upelelezi, ushahidi au kuleta hofu kwa jamii. Mjue taarifa za uhalifu hazina budi kukusanywa, kuchambuliwa na kutolewa kwa makini bila kukurupuka.”
Aidha amesema Jeshi hilo lipo tayari kushirikiana na wanahabari katika mapambano dhidi ya uhalifu nchini.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA