February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

NYARAKA ZA PANDORA: FAMILIA YA UHURU KENYATTA YADAIWA KUFICHA MALI PANAMA

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mama yake ni miongoni mwa viongozi duniani waliotajwa kwenye nyaraka za Pandora kuwa wanamiliki akaunti za siri Panama. Pia ndugu zake watatu, wanamiliki kampuni tano za nje ya nchi  zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 30.Hatahivyo  Kenyatta na familia yake hawakujibu maombi ya ICIJ ya kutoa maoni yao juu ya taarifa hizo.

Mali hizo za siri zilifichuliwa na uchunguzi, uliochapishwa mapema siku ya Jumapili, na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi (ICIJ), Finance Uncovered , Africa Uncensored na mashirika mengine ya habari.

Nyaraka za Pandora ni uvujaji wa hati na faili karibu milioni 12 zinazoonyesha utajiri wa siri wa viongozi, wanasiasa na mabilionea. Kulingana na uchunguzi huo wa ICIJ, Nyaraka za Pandora zinaonyesha kuwa watu wenye vyeo vya ngazi za juu ambao wangeweza kusaidia kukomesha wa kukwepa kodi badala yake wananufaika nao.

 Kwa kutumia mfumo huo wanahamisha mali kwenye kampuni za siri na huku serikali zikishindwa kupunguza kasi ya mtiririko wa pesa haramu ulimwenguni ambao unatajirisha wahalifu na kuongeza umaskini katika mataifa duni.`

Kulingana na ICIJ, Bi Kenyatta na binti zake walishauriwa na wataalamu wa utajiri wa kimataifa kutoka benki ya Uswisi, ambayo iliajiri Alcogal, kampuni ya mawakili ya Panama iliyobobea katika kuanzisha na kusimamia kampuni za pwani na hati za malipo kutoka Alcogal kwenda benki zinaonyesha kuwa washauri wa Uswisi waliwataja familia ya Kenyatta kutumia nambari ya “mteja 13173”.

Alcogal ilitoa ofisi iliyosajiliwa kwa Milrun katika visiwa vikubwa zaidi vya BVI, Tortola, na kuwapa wafanyakazi kufanya kazi kama wakurugenzi rasmi wa kampuni hiyo.Matokeo yake ilikuwa kampuni isiyojulikana kabisa ambayo haingeweza kuhusishwa na familia ya Kenyatta.

Kampuni hiyo inelezwa kuwa  ilitumiwa na Bi Kenyatta na binti zake kununua nyumba katikati mwa mji wa London, ambayo bado inamiliki, kulingana na stakabadhi kwenye ofisi ya Usajili wa Ardhi ya Uingereza zilizotazamwa na Finance Uncovered.

Kulingana na taarifa za  Finance Uncovered, familia ya Kenyatta imetumia kampuni zingine zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru kununua mali mbili zaidi nchini Uingereza.Washauri wa utajiri wa kibinafsi wa UBP pia walisaidia kaka wa Bw Kenyatta, Muhoho, kuanzisha shirika la Panama linaloitwa Criselle Foundation mnamo 2003.

Viongozi wengine waliotajwa katika nyaraka za Pandora ni pamoja na Mfalme wa Jordan Abdullah II, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba na Rais wa Congo-Brazzaville Denis Sassou-Nguesso.