February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

NIGERIA : WATEKAJI WAMTEKA MZEE ALIYEBEBA KIKOMBOZI

Waswahili husema mjumbe huwawi lakini huko nchini Nigeria watekaji nyara wamemteka mwanaume aliyetumwa kupeleka malipo ya fidia (kikombozi)  ili kuachiliwa kwa watoto wa shule waliotekwa nyara.

Mzee huyo alitumwa na wazazi wa watoto hao baada ya kufanikiwa kukusanya naira  30 baada ya kuuza ardhi na mali zingine ili waweze kuwakomboa watoto hao katika mikono ya watekaji nyara.

Inaelezwa kuwa watu sita walitumwa na kiwango sahihi walichokitaka watekaji hao ili kukutana na watekaji nyara karibu na msitu ambao watoto walikuwa wakishikiliwa na walipofika, watu hao waliojihami kwa silaha walimtaka mmoja wa kikundi hicho awafuate msituni ili pesa zihesabiwe.

Na baadayw watekaji hao walipiga simu kudai kuwa pesa zilizotolewa sio kiwango walichokubaliana na kuendelea kumshikilia mateka mzee huyo aliyebeba kikombozi huku wazazi wa watoto hao wakiachwa hawajui hatma ya tukio hilo.

Takribani wanafunzi 136 walitekwa nyara kutoka shule ya Kiislamu huko Tegina, jimbo la Niger, mwishoni mwa mwezi Mei ambapo watu wenye bunduki waliokuwa wamepanda pikipiki walivamia mji huo na kuanza kufyatua risasi kiholela na kumuua mtu mmoja huku mwingine alijeruhiwa na wakati watu wakikimbia, watekaji hao walikwenda shuleni na kuwakamata watoto hao.