March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

NI MIAKA MITANO SASA TOKEA LISSU ASHAMBULIWE

Je, wajua?, Mnamo Septemba 7, 2017 (tarehe kama ya leo), Mwanasiasa ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliripotiwa kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa kwenye gari lake kuelekea kwenye makazi yake Jijini Dodoma.

Baada ya tukio hilo Tundu Lissu alipekwa Nchini Kenya ili kupatiwa matibabu kufuatia kupata majeraha ya risasi na badae kwenda Ubelgiji kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mwanasiasa huyo alirejea Nchini kipindi cha uchaguzi Mkuu 2020 ambapo alikuwa akipeperusha bendera ya CHADEMA katika kinyanganyiro cha Urais, lakini siku chache baada ya zoezi la uchaguzi kukamilika akishika nafasi ya pili nyuma ya Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alitangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) aliondoka kurudi tena Nchini Ubelgiji huku akidai kuwa bado anahofia usalama wake.

Jeshi la Polisi kupitia IGP, Simon Sirro ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Balozi Nchini Zimbabwe limekuwa likitoa taarifa kuwa usalama upo.(alisema kipindi akiwa IGP)

Siku chache baada ya Lissu kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan mnamo mwezi February mwaka huu, Rais Samia alifanya mahojiano na chombo cha habari na kueleza kuwa usalama upo nchini na wale wote wanaodai kukimbilia nje ya Nchi wanakaribishwa. Rais Samia alitoa majibu hayo kutokana na swali lililohoji sababu anayoitoa Lissu na wenzake kuhusu kohofia kurejea Nchini Tanzania.

Siku chache baada ya kauli hiyo Tundu Lissu alisikika alitoa ahafi ya kurejea nchini kuendelea na shughuli za kisiasa, huku akisisitiza kufanyika kwa upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwake.

Jeshi la Polisi limekuwa likieleleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo hauwezi kuachwa badala yake wanaitaji ushirikiano zaidi kutoka kwa Lissu ili kukamilisha uchunguzi huo na hatua nyingine kufuata.

Itakumbukwa Tundu Lissu ni miongoni wanasheria maarufu nchini na wakati anakumbana na tukio la kushambuliwa alikuwa akihudumu katika nafasi ya Ubunge Katika jimbo la Singida Mashariki. Lisu pia amewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), amekuwa mkosoaji na mshauri wa masuala mbalimbali hususani kisheria ikiwemo mikataba ambayo imekuwa ikisainiwa na Serikali, Katiba na kanuni mbalimbali ambazo hutungwa na Serikali.

Imetolewa na Watetezi TV
7/9/2022