February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

NGORONGORO :SITA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KUWEPO TANZANIA KINYUME CHA SHERIA

Watu SITA wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Ngorongoro hii leo Julai 11,2022 kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume cha sheria.

Akisoma mashitaka yao mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Loliondo,Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji,Shija amesema mnamo Juni 6 mwaka huu majira ya mchana watuhumiwa walikutwa katika Wilaya ya Ngorongoro bila kuwa na hati ya kusafiria pamoja na vibali vya ukaazi vinavyowaruhusu kuishi Tanzania, kinyume na Kifungu cha 45(1)(i) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Loliondo,Mhe. Malisa amewataka watuhumiwa hao kutojibu lolote kwakuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuchukua ukiri wao, hivyo ameahirisha shauri hilo hadi Julai 13 mwaka huu ambapo washitakiwa hao watasomewa upya mashitaka yao mbele ya Hakimu Wa Mahakama ya Wilaya Ngorongoro.

Aidha Mhe.Malisa ameongeza kuwa masharti ya dhamana katika shauri hilo namba 16/2022 yatawekwa na Hakimu wa mahakama ya Wilaya hivyo watuhumiwa wataendelea kukaa rumande hadi Julai 13/2022.

Wanaoshitakiwa katika shauri hilo namba 16/2022  ni Samson Kapukya,Philip Mwiori,Sarirya Kelembu,Dominic Leturi,Melua Sitaka Maco na Saruni Ololopa Koliata.

Wakati huo huo Rebeka Koriata Jacob na Mume wake Jacob Ormunai Koriata wamefikishwa katika mahakama hiyo ya Wilaya ya Ngorongoro kwa tuhuma mbalimbali.

Mshitakiwa namba moja katika shauri hilo namba 17/2022 Rebeka Jacob Koriata amesomewa mashitaka mawili ikiwemo la kuwepo nchini Tanzania kinyume cha sheria ya uhamiaji ambapo Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji,Shija amesema mshitakiwa akiwa ni Raia wa Kenya mnamo Juni 29 mwaka huu alikutwa katika kijiji cha Olorosokwani wilayani Ngorongoro akiwa hana hati ya kusafiria au kitambulisho cha ukaazi kinachomruhusu kuwepo Tanzania.

Katika shitaka la Pili mshitakiwa anadaiwa kufanya kazi ya uhasibu bila kuwa na kibali kinyume cha kifungu cha 45(1)(m) na (2) cha Sheria ya uhamiaji.Mnamo Juni 29,2022 mshitakiwa akiwa ni Raia wa Kenya, alikutwa katika kijiji cha Orogorosok wilayani Ngorongoro akifanya kazi ya uhasibu katika shirika lisilo la kiserikali la Maasai Honey tangu Julai mosi mwaka 2021 bila kibali kinachomruhusu kufanya kazi Tanzania.

Shitaka la tatu linalomkabili mshitakiwa wa kwanza,Rebeka Koriata anadaiwa kujihusisha na kufanya kazi ya uhasibu bila kuwa na kibali rasmi kilichoidhinishwa kinyume na kifungu cha 9(1),(2) na (3)cha “The Non-Citizens (Employment Regulation) Act.Inadaiwa mtuhumiwa akiwa sio mtanzania mnamo Juni 29,2022 alikutwa na maafisa wa Uhamiaji katika kijiji cha Orogosorok wilayani Ngorongoro akifanya kazi ya uhasibu katika Shirika lisilo la kiserikali la Maasai Honey tangu mwaka 2021 bila kuwa na kibali cha kazi au cheti kinachomruhusu kufanya kazi Tanzania.

Shitaka la tatu linamkabili, Mshitakiwa wa pili katika shauri hilo namba 17/2022 Jacob Ormunai Koriata anadaiwa kumhifadhi mhamiaji haramu kinyume cha kifungu cha 45(1) (l) na (2) cha sheria ya Uhamiaji.Jacob Koriata anadaiwa kumhifadhi raia wa Kenya Rebeka Koriata ambaye amekuwa akiishi nae kama mke tangu mwaka 2016 akijua ya kwamba ni raia wa Kenya na hana kibali cha kuishi Tanzania.

Katika shitaka la tano, Jacob Koriata anashitakiwa kwa kumsaidia mshitakiwa Rebeca Koriata kutenda kosa la kuwepo nchini kinyume cha sheria ya uhamiaji kwa kuishi nae kama mke tangu mwaka 2006 akijua kuwa ni raia wa Kenya na hana hati ya kusafiria au kibali cha kumruhusu kuishi Tanzania.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Loliondo,Malisa amewataka washitakiwa hao kutokujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuchukua ukiri wao.Hivyo ameahirisha kesi hiyo mpaka Julai 13 mwaka huu ambapo washitakiwa hao watasomewa mashitaka upya mbele ya Hakimu wa mahakama ya Wilaya Ngorongoro.Washitakiwa wote wamerudishwa rumande.

Washitakiwa wote katika kesi hizo mbili wamewakilishwa na Wakili Richard Moshi na wakili Lucas Julius Lukumay.