February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

SERIKALI: WATANZANIA WAISHIO UKRAINE WAPO SALAMA , ACT-WazalendoYATAKA WAREJESHWE HARAKA

Na Mwandishi wetu

Serika ya Tanzania, imesema Watanzania  waishio nchini Ukraine, wako salama , huku ikiwataka wananchi kuwa watulivu wakati inawasiliana na mamlaka za nchi hiyo, ili kuhakikisha hawapati madhara.

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, tarehe 25 Februari 2022 na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buholela.

Ni siku moja baada ya Rais wa Ukraine, Volodomyr Zelenskky, kutangaza hali ya hatari, kufuatia Taifa lake kuvamiwa na vikosi vya kijeshi vya Urusi.

” Serikali ya Tanzania inapenda kuujulisha umma wa Watanzania kuwa, hadi sasa hakuna Mtanzania aliyepata madhara yoyote kufuatia hali inayoendelea nchini Ukraine na kusababisha Serikali ya nchi hiyo kutangaza hali ya hatari tarehe 24 Februari 2022,” imesema taarifa ya Buhohela.

Kupitia taarifa hiyo, Serikali ya Tanzania imewataka Watanzania waishio Ukraine, kuwasiliana na Ubalozi wake nchini Sweden, huku ikiwataka wafuate maelekezo ya Serikali ya nchi hiyo.

“Serikali inawashauri Watanzania kufuata na kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na Serikali ya Ukraine kwa raia wasiokuwa raia wa nchi hiyo. Kuendelea kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, ambao pia unawakilisha Ukraine kwa jambo lolote la dharura kwa kufuata utaratibu wa mawasiliano uliotolewa na ubalozi,” imesema taarifa ya Buholela na kuongeza:

“Serikali inawaomba Watanzania wote waishio Ukraine kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kufuatilia usalama wao, kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Ukraine. Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu hali za Watanzania waishio Ukraine.”

Wakati Serikali ya Tanzania ikitoa taarifa hiyo, Chama chaACT-Wazalendo, kupitia Naibu Msemaji wake wa Kisekta wa Mambo ya Nje, Dahlia Majid Hassan, kimeitaka kuchukua hatua za dharura kuwarejesha nyumbani Watanzania waishio Ukraine na Urusi.

“ACT Wazalendo kinaitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha Watanzania walioko nchi za Ukraine na Russia, wanakuwa salama kipindi hiki cha mgogoro wa kivita ulioibuka na kuanza kusababisha maafa baina ya nchi hizo mbili,” imesema taarifa ya Hassan na kuongeza:

“Kulinda raia na kuhakikisha usalama wao ni jukumu la mwanzo na la kipaumbele kwa taifa lolote, wakati na mahali popote wanapokuwa katika hatari hasa inapotokea majanga kama haya ya vita.”