December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MZEE WASIRA ATAKA RAIS SAMIA ASILAUMIWE PANDAJI BEI YA MAFUTA

Waziri wa zamani nchini Tanzania, Mzee Stephen Wasira, amesema wanaohoji kwa nini Rais Samia Suluhu Hassan, hadhibiti kupanda kwa bei ya mafuta, wanamtishwa mzigo kwa kuwa hana uwezo wa kudhibiti mfumuko huo katika soko la dunia.

Kauli hiyo imetolewa na Mzee Wasira, leo Jumamosi, akichangia mada katika mdahalo wa kitaifa wa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyere, iliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini Tanzania, amesema kupanda kwa bei ya nishati hiyo, kumesababishwa na mgogoro wa kivita kati ya Urusi na Ukraine.

“Kukiwa na upungufu wa mafuta duniani bei zinapanda, ukisema Rais Samia kwa nini hasimamii mafuta, hii sasa unamtwisha mzigo, lakini naamini kila tunapoendelea kujifunza, tunajua nani ni nani na nini ni nini,” amesema Mzee Wasira.

Mzee Wasira amesema, Rais Samia bado ana kazi ya kufanya katika kukabiliana na changamoto hiyo, kwani hana uwezo wa kuizuia.

“Wakati Rais Samia anajitahidi sana kwenda na sera ya maendeleo ya watu, kwa sababu maendeleo lazima yawe ya watu, ndiyo maana mkazo wake uko katika mifumo inayozingatia maendeleo ya watu. Lakini bado ana kazi ya kufanya, kuna Ukraine na Urusi inapandisha bei ya mafuta,” amesema Mzee Wasira na kuongeza:

“Ukienda mtaani wanadhani Samia ndiye anaanzisha vita, kwa hiyo wanasema kwa nini bei hasimamii, Samia atasimamia bei lakini hawezi kuzuia kupanda kwa mafuta, sababu Urusi inayopigana ni ya tatu kutoa mafuta duniani ikishindwa kuuza sababu ya vikwazo kuna kuwa na upungufu wa mafuta na bei zinapanda.”