February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MZEE WARIOBA AONESHA NJIA UFUFUAJI MCHAKATO KATIBA MPYA

Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba, ameshauri Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2011, ifanyiwe marekebisho yakayowezesha uundwaji wa kamati ya wataalamu, watakaokamilisha mchakato wa upatikanaji katiba mpya.

Jaji Warioba ametoa ushauri huo leo Jumanne, jijini Dodoma akihutubia katika kongamano la haki, amani na maridhiano, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Mwanasiasa huyo amesema, tayari kazi kubwa imeshafanyika katika mchakato huo, ikiwemo ufanyikaji bunge maalumu la katiba, lililopitisha katiba pendekezwa, kisha tume ilikusanya maoni ya wananchi yaliyoandaa rasimu ya katiba.

Amesema mchakato wa katiba mpya hauna haja ya kurudishwa bungeni, kwani hatua iliyobaki ni ya wananchi kupiga kura dhidi ya katiba pendekezwa.

“Sheria ile inaweza kubadilishwa ukapata utaratibu wa kusahihisha yaliyomo humu, mahali ambako kuna mapungufu mengi kunaweza kuwa na kamati ya wataalamu. Nenda bungeni weka mabadiliko kwenye sheria yaruhusu kuwe na kamati,” amesema Jaji Warioba.

Jaji Warioba amesema kamati hiyo itafanya kazi ya kulinganisha rasimu ya katiba, iliyobeba maoni ya wananchi na katiba pendekezwa. Kisha itatoa mapendekezo ambayo yatakwenda kupitishwa bungeni.

“Mapendekezo hayo yaje kwa viongozi wa kisiasa wakae wayajadili, wakiyajadili yakikubalika inaweza ikapelekwa bungeni, iukapitishwa,” amesema Jaji Warioba.

Aidha, Jaji Warioba amekosoa mapendekezo ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia, kuhusu mchakato wa upatikanaji katiba mpya, kuanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Jaji Warioba amesema ajenda zinazowahusu wananchi ambazo zinapaswa kuingizwa katika marekebisho hayo, haziwe kusubiri uchaguzi mkuu.

“Katika rasimu ya katiba, wananchi walikuwa na mambo yao ya muhimu kabisa, moja ilikuwa haki za binadamu, katika mazungumzo yale walisistiza sana haki za binadamu, walisema kwanza hizi zilizopo mzisafishe zina vizuizini mno, ziwe haki sawa,”

“ Hamuoni kuna umuhimu mnasema hio lingojee mchakato uje baada ya uchaguzi? Yaani tusitambue haki za binadamu mpaka tufanye mchakato?” amesema Jaji Warioba.