February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MZEE WA MIAKA 80 AFIKISHWA MAHAKAMANI KUDAIWA URITHI NA MTOTO BAADA YA KUOA

Mzee Farid akitoka Mahakamani leo June 22.

Mzee Kharid Segeleje (80) mkazi wa kijiji cha Mwamgongo wilaya ya Kigoma amefikishwa katika mahakama ya wilaya na mtoto wake wa kuzaa anaedai urithi,katika kesi ya madai ya mirathi namba 8 ya mwaka 2021 iliyosikilizwa na Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Kenneth Mutembei.

Mbele ya mahakama hiyo, mtoto wa mzee huyo, Abbas Kharid amesema anahitaji urithi wa mali za baba yao kutokana kutokunufaika nazo kwa sasa baada ya mama yao kufariki na mzee huyo kuoa mwanamke mwingine ambaye ndiye amekuwa akinufaika pamoja na watoto wake .

Awali kesi hiyo ilisikilizwa katika mahakama ya mwanzo ya Kalinzi ambayo ilimpa ushindi mzee huyo kabla ya watoto kutoridhika na uamuzi wa mahakama uliowapelekea kukata rufaa katika mahakama ya wilaya.Mali zilizoelezwa ni nyumba na shamba la michikichi lenye ukubwa wa hekari 20

Baada ya maelezo ya shauri hilo kusikilizwa,wakili wa upande wa utetezi Thomas Msasa, amesema ameamua kumsaidia mzee huyo katika utetezi mahakamani ili apate haki yake.

“Naamini hakuna mahakama inaweza kumnyima mzee huyu haki yake “Alisema.

Baada ya kupokea maelezo hayo hakimu Mutembei akasema kesi hiyo itaendeshwa kwa njia ya maandishi hivyo upande wa mlalamikaji watatakiwa kuwasilisha hoja zao kwa maandishi tarehe 28/6/2021 na upande wa utetezi mnamo tarehe 05 July utatoa majibu ya hoja hizo na 12 July watafika mahakamani hapo kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya hukumu.