February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MWANAFUNZI ADAIWA KUUAWA NA KUNYOFOLEWA SEHEMU ZAKE ZA SIRI

Na: Anthony Rwekaza

Kufuatia kuwepo kwa madai ya taarifa ya kuuawa kwa Mwanafunzi Mkoani Tabora, Kamanda wa Polisi katika Mkoa huo, Kamishna Msaidizi (ACP) Richard Abwao, amethibitisha uwepo kwa tukio hilo, linalodai mwanafunzi kuuawa na kunyofolewa viungo vyake vya sehemu za siri.

Kamanda huyo amekili kupokea taarifa hizo na amehidi kukutana na waandishi wa habari ili kulizungumzia zaidi suala hilo ambalo limeibua hali sintofahamu hususani familia na ndugu na jamaa wa mtoto huyo.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Ngassa Kazungu, alisema jana Januari 1, 2022, kuwa Maria baada ya kutoka shuleni majira ya saa kumi na moja jioni aliagizwa na Mama yake kwenda kuchota maji kisimani.

Mzazi huyo ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza mwanawe huyo alifuata maji na kurejea nyumbani salama lakini aliporudia kwa mara ya pili hakuonekana hadi siku ya pili mwili wake ulipookotwa kwenye kichaka ukiwa umenyofolewa viungo vyake katika sehemu ya siri na masikio yakiwa yametobolewa.

‘’Nimepata pigo ambalo sitalisahau katika maisha yangu kwani mtoto wangu Maria ameuawa kikatili na mimi niliamua kumsomesha mwanangu ili siku za mbeleni aje kunisaidia lakini wameamua kukatisha maisha yake,” amesema Ngassa Kazungu

Kufuatia tukio hilo Kazungu amesema anamwachia Mungu pamoja na Jeshi la Polisi kwa kuwa mauaji kama hayo hayapaswi kufumbiwa macho na vyombo vinavyohusika, huku akisisitiza kuwa kuna ulazima tukio hilo lifanyiwe kazi ili kuwabaini wanaofanya unyama kama huo.

Pia kwa upande wa Mwenyekiti wa Serikali Kitongoji cha Ulula, Masele Charles alikiri kuuawa kwa mwanafunzi huyo na kuwa amesikitishwa tukio hilo, pia Mwenyekiti huyo aliweka bayana kuwa hivi sasa anategemea kuanza kuanzisha utaratibu wa ulinzi mkali wa jeshi la sungusungu na polisi jamii katika kitongoji chake ili kukabiliana na vitendo vya mbalimbali vya uhalifu.

Aidha Diwani wa Kata ya Tutuo, Rashidi Magope, alionya waliofanya tukio hilo licha ya bado kuwa hawajulikani, amedai pia walimtoboa mara tatu sikio la mkono wa kulia na ameongeza kwamba tukio hilo la kuuawa kwa mwanafunzi huyo ni la pili kwa kuwa hata mwaka jana 2021 iliripotiwa kuawa kwa mwanafunzi wa shule ya sekondari.

Diwani huyo aliongeza kuwa mauaji hayo yanaleta taswira mbaya katika Kata yake na hivyo amewataka baadhi ya wananchi wanaojihusisha na vitendo kama hivyo kuacha mara moja, huku akiliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wahusika wa uhalifu huo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua zaidi.