March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MWAKA MMOJA WA SAMIA MADARAKANI: DK. NCHEMBA ASEMA FEDHA ZIMERUDI MTAANI

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mzunguko wa fedha ‘Ukwasi’, umeongezeka kwa wastani wa asilimia 9.3.

Waziri huyo wa fedha, ametoa taarifa hiyo leo Jumanne, jijini Dodoma, akitoa taarifa ya mafanikio ya Serikali hiyo, iliyoingia madarakani Machi 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

“Mzunguko wa fedha katika uchumi umeongezeka kwa wastani wa asilimia 9.3, hii na yenyewe si namba kwenye karatasi, sote tunajua Sh. 1.3 trilioni zilizotolewa na IMF zilikwenda katika ujenzi wa madarasa vijijini, hivyo imeenda kwenye mzunguko wa fedha ndani ya nchi,” amesema Dk. Mwigulu.

Dk. Mwigulu amesema “ndiyo maana sherehe za Krismasi na mwaka mpya ilikuwa maeneo mengi ukienda, lazima kwanza uombe kiti cha nyongeza. Kulikuwa hakuna pa kukaa kila eneo limejaa, sababu watu wana ukwasi.”

Akielezea mafanikio mengine ya Serikali hiyo, Dk. Mwigulu amesema mikopo ya sekta binafsi imeongezeka kutoka asilimia 3.3 , iliyokuwa Desemba 2020, hadi 10, wakati mikopo chechefu katika sekta ya mabenki ikipungua kutoka asilimia 9.3 hadi 8.2.

“Kupungua mikopo chechefu inatokana na Rais Samia kuagiza wazabuni wanaoidai Serikali walipwe. Wengi mitaji yao walikopa kwenye benki na alipopata wakaenda kuilipa,” amesema Dk. Mwigulu.

Dk. Mwigulu amesema akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kutoka Dola za Marekani 6.0 bilioni, hadi 6.4 bilioni.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu amesema mapato ya Serikali yameongezeka hadi kufikia Sh. 15.7 trilioni, huku ya Desemba yakivunja rekodi ambapo yalikuwa Sh. 2.5 trilioni.