February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MUSWADA SHERIA YA KULINDA FARAGHA, DATA WATUNGWA

Serikali ya Tanzania, imesema imetunga muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ili kudhibiti vitendo vya uvuvjaji wa mawasiliano ya watu mitandaoni.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika jijini Dar es Salaam, uliokuwa na lengo la kutaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2022.

“Lakini muswada wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi uko kwenye hatua za mwisho. Tumeshafanya mchakato ndani ya mwaka mmoja. Hii sheria  ni  ya muhimu kwa sababu vinginevyo uwekezaji utakuwa mgumu,” amesema Nape.

Nape amesema “ kelele zimekuwepo za muda mrefu na ni kelele ya dunia, lazima tuwe na protection (ulinzi), sio kwa sababu kulikuwa na kurekodi rekodi watu hapa,  hapana. Lakini ni kwa sababu ya kutunza privacy (faragha) ya watu.”

Akielezea mafanikio ya wizara yake, Nape amesema katika kipindi hiko imefanikiwa kuzifanyia marekebishi sheria mbalimbali, ikiwemo ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010.Sheria ya Shirika la Posta ya 1993.

Mbali na marekebisho ya sheria hizo, Nape amesema wizara yake ilizipitia na kufanya marekebusho sera kadhaa, hasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Sera ya Utangazaji ya 2003 na Sera ya Posta ya 2003.

Nape amesema mafanikio mengine ni urekebishaji wa kanuni zinazosimamia tasnia ya habari na mawasiliano pamoja na kuyafungulia mageti yaliyofungwa, ikiwemo la MwanaHALISI, Mawio na Tanzania Daima.