March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MTOTO WA MIAKA 7 ADAIWA KUBAKWA NGORONGORO

Mtoto wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka saba (Jina limehifadhiwa) anadaiwa kubakwa na kijana mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 25 hadi 30 majira ya jioni wakati akitoka shule, huko Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, mwezi Februari mwaka huu.


Kwa mujibu wa Ushahidi wa mtoto huyo alipokuwa katika mahakama ya wilaya ya Ngorongoro aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio majira ya jioni alipokuwa akitoka shuleni alikutana na kijana ambaye alimuita kwa nia ya kutaka kumtuma dukani, na alipofika eneo hilo ili kuitikia wito na kuchukua pesa ndipo kijana huyo alipomvuta na kuanza kumvua nguo na kisha kuanza kumfanyia kitendo hicho cha ubakaji huku akimtishia kuwa akipiga kelele atamuua.
Wazazi wanasema waligundua utofauti kwa binti yao hasa baada ya kumuona akiwa katika hali ya unyonge jambo ambalo sio la kawaida na baada ya kumhoji alikiri kuingiliwa kimwili.


Baada ya mahojiano wazazi hao walimchukua mtoto huyo hadi shuleni anakosoma ili kuonana na waalimu, kisha wakamchukua mtoto huyo hadi hospitali kwa ajili ya uchunguzi Zaidi na kubaini kuwa ni kweli mtoto huyo alikuwa ameingiliwa kimwili.


Hata hivyo kesi hiyo inadaiwa kugubikwa na sintofahamu hasa baada ya wazazi wa mtoto huyo kuwalalamikia manesi kwa kupoteza Ushahidi wa Ripoti ya awai ya uchunguzi wa kitabibu (PF3) iliyotolewa na Hospitali iliyothibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kulazimika kutoa ripoti nyingine mbili tofauti ambazo zina maelezo tofauti na ripoti ya awali. Imeelezwa kuwa baada ya kipimo hicho kupotea ilibidi vipimwe vipimo vingine viwili tofauti huku kipimo cha tatu kikichukuliwa baada ya siku 10 tangu kutokea kwa tukio hilo.


Taarifa zinadai kuwa hilo sio tukio la kwanza kutokea katika eneo hilo huku wakazi wa maeneo hayo wakiendelea kuyafumbia macho matukio hayo na kuona aibu kuyaripoti suala ambalo limeendelea kuchochea ongezeko la matukio ya ubakaji walayani Ngorongoro.


Mpaka sasa kesi hiyo ipo katika Mahakama ya Wilaya Ngorongoro na imeahirishwa hadi tarehe 18 Mei, mwaka huu itakaposikilizwa tena.