March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MSHITAKIWA NAMBA MBILI KESI YA MBOWE NA WENZAKE ATOA USHAIDI, AELEZA ALIVYOKAMATWA, KUENDELEA KUTOA USHAIDI SEPTEMBA 27, 2020

Na Hilda Ngatunga

Mshitakiwa namba mbili katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake, Adam Kasekwa(anayedaiwa kuwa alikuwa komandoo wa JWTZ) ameieleza Mahakama kuwa ACP Ramadhani Kingai alimpatia nyaraka ambazo hakufahamu zimeandikwa kitu gani na kumlazimisha asaini na kuandika maelezo ya uthibitisho hivyo alifanya kama alivyoamriwa na Kingai.

“Kingai na Goodluck walinitoa mahabusu wakanipeleka kwenye chumba kina viti viwili na meza mbili,Goodluck akasimama mlangoni,Kingai akaniambia hapa uwe mstaarabu tunakufungua pingu kuna nyaraka ambazo tumekuja nazo tunataka usaini.’

Adam Kasekwa ameeleza hayo hii leo Septemba 24, 2021 wakati akitoa ushahidi wake mahakamani katika shauri dogo la kesi ya msingi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Mshitakiwa huyo amesema alivamiwa na kikundi cha watu watano katika eneo la ‘Rao madukani’ ambapo mmoja alimkaba kwa nyuma na mwingine akatoa silaha na madawa na kuingiza kwenye maungo yake na kuyatoa,kisha alimsikia mtu huyo akisema amemkuta na madawa na silaha.na kuiambia mahakama kuwa hakukamatwa bali alitekwa.

“Walionivamia wengine wamenikaba mmoja akaja na yake madawa akawa ameyabana kwenye nguo alafu akatoa akasema ana madawa,mwingine akaja akanibana kwa nyuma akaweka mkono akatoa akasema ana sialha,” alisema Kasekwa.

Mshitakiwa huyo amesema katika zoezi hilo la ukamataji hakuona mashahidi huru wawili kama walivyotajwa na mashahidi wa upande wa Jamhuri ACP Kingai na Inspecta Mahita wakati wakitoa ushahidi wao mahakamani.

Ameiambia Mahakama baada ya kuona hivyo mshitakiwa wa tatu,Mohamed Ling’wenya ambaye kwa wakati huo walikuwa wote alijihami na kutoa vitu vyake vyote alivyokuwa navyo mfukoni ili asiwekewe madawa hayo kama alivyowekewa yeye (Kasekwa) .Pia ameionyesha mahakama suruali aliyovaa siku ya tukio ikiwa ina hook moja baada ya zingine kukatika wakati anakamatwa.

Ameendelea kuieleza Mahakama kuwa wakati anakamatwa alikuwa na simu ndogo aina ya Itel yenye line moja ya Airtel na pesa taslimu Kiasi cha Sh.260,000, ambapo Askari aliyemtaja kwa jina la Goodluck alichukua wakati anampekua na kumkabidhi ACP Ramadhani Kingai hata hivyo tangu wakati huo hafahamu fedha hizo zipo wapi na hakupewa risiti.

Alipoulizwa na Wakili wake John Mallya kama aliwafahamu waliomkamata alisema aliwafahamu baadhi baada ya kujitambulisha wakati wakitoa ushahidi wao mahakamani, akiwemo Inspecta Omari Mahita na ACP Ramadhani Kingai na hawakumuonya wakati wanamkamata na hawakuwa na notebook ambayo wangetumia kurekodi.

Mshitakiwa huyo ameiambia mahakama kuwa baada ya kukamatwa waliwekwa kwenye gari na kuanza kupigwa na kuteswa na hawakufahamu wanaenda wapi hadi walipofikishwa kituoni na alikuja kufahamu kuwa kilikuwa ni Kituo cha Moshi ‘Central Police’ wakati walipokuwa wakitoa ushahidi mahakamani.

Akiendelea kutoa ushahidi wake amesema baada ya kufikishwa kituoni hapo alitolewa mahabusu na kupelekwa kwenye vyumba vya pembeni ambapo aliculiwa nguo zote na kufungwa pingu mikononj na miguuni na kisha walichukua chuma na kumnin’giniza mithili ya popo anavyokaa na baada ya hapo walianza kumpiga.

“Niliulizwa swali huku Moshi umefuata nini nikawajibu nimekuja kusaini mkataba wa VVIP Protection kwa Mbowe,jibu hili halikuwaingia akilini waliendelea kunipiga wakiniuliza swali hilo hilo,” ameieleza mahakama.

Amesema baada ya kupigwa kwa takrbani daikika 45 alifunguliwa pingu na kuvalishwa suruali huku shati akiwekewa begani na amedai walianza kumkokota kwani alikuwa hawezi kutembea na akafungwa pingu za mikononi na kupelekwa mahabusu na tangu walipofikishwa kituoni hapo hakufahamu hatma ya mshitakiwa mwenzake Mohamed Ling’wenya.

“Niliendelea kukaa selo hawakunitoa tena,ilipofika jioni alikuja askari mmoja akamwaga maji mle na kuniacha,ilipofika kesho yake niligundua ni mchana walinitoa kwa kunikokota ingawa walinilazimisha nitembee ila ilikuwa ni kwa shida,” ameeleza.

Akiendelea kutoa ushahidi wake amesema baada ya kutolewa nje alifungwa Jacket lake usoni na kupandishwa kwenye gari ingawa hakufahamu anapelekwa wapi ambapo walimchoma na bisibisi eneo la mbavu na makalio huku wakimwambia wanakokwenda ndio mwisho wa maisha yake.

“Safari ilikuwa ya muda mrefu kwenye gari sikukaa kwenye siti nilikaa chini gari ilikuwa inachemka niliungua muda wote,safari ilikuwa ya muda mreu sana tukaja tukashushwa wakaniburuta wakaniingiza kwenye chumba wakanitoa lile Jacket ,wakafunga mlango wakaniacha nikiwa na pingu” amesema mshitakiwa namba 2.

Pia ameieleza mahakama kuwa alikuja kufahamu kuwa yupo katika kituo cha Polisi TAZARA baada ya kuwauliza mahabusu waliokuwa katika chumba kingine na pia alisikia mlio wa honi ya Treni.

Amesema alikaa kituoni hapo toka tarehe 7/08/2020 na ilipofika tarehe 10/08/2020 alfajiri alichukuliwa akiwa amefungwa pingu na kufungwa Jacket usoni na kwa siku hiyo aliweza kutembea kwa kuchechemea.

“Walipoona naweza kutembea wakaniambia jiandae huko unapokwensa yatakukuta tena yaleyale.Nikapandishwa kwenye gari haikuchukua muda sana nikashushwa wakaniingiza ndani wakanifungia kwenye chumba,”

Akiongozwa na Wakili wake John Mallya kuonyesha uthibitisho kuwa aliteswa,Mshitakiwa Adam Kasekwa aliionyeaha mahakama makovu katika goti la mguu wa kushoto na mkono wa kushoto na kueleza kuwa mpaka sasa bado ana maumivu ya mguu kwani tangu alipokamatwa hakupatiwa matibabu.

Pia ameieleza mahakama kuwa hakupewa chakula aina ya Nyama choma na Energy na yeye huwa hatumiagi kinywaji hicho zaidi ya soda.Aidha ameeleza wakati akitiwa nguvuni waliomkamata hawakujitambulisha kwa majina au kuelezwa mashitaka yake ma aliwafahamu baadhi kwa majina walipojitambulisha mahakamani.

Akipngozwa na Wakili wake amesema hakushiriki katika zoezi la kumtafuta mshitakiwa mwingine aliyetajwa kwa jina la Moses Lijenje na wakati wote alikuwa amefungwa pingu na kuteswa.

Kasekwa ambaye alikuwa askari wa JWTZ kikosi cha 92 KJ akiwa kama komandoo na alihudumu kwa miaka sita kabla ya kuachishwa kazi kwa sababu za kiafya.Amesema alikuwa mmoja wa askari walioshiriki mission ya kulinda amani nchini Congo mwaka 206-2017 na baada ya kurudi nchini alipatwa na linaloathiri mfumo wa akili la Battle confusion.

“Nilirejea kazini kama kawaida na wakuu wangu wakagundua nna tatizo la Battle Confusion na ni kitu kinachoweza kumpata askari yotote unapokuwa katika majukumu mazito milio ya risasi,mizinga sana akili haiendi kama wakubwa wanavyotaka,”amesema

Akiendelea kutoa ushahidi wake Kasekwa amesema alifikishwa kituo cha polisi Mbweni na kupewa kikaratasi chenye jina la Vicent Juma na kupewa maagizo ya kutumia jina hilo atakapoulizwa.

“Walinikabidhi kikaratasi kuwa jina langu ni Vicent Juma na una kesi ya unyang’anyi na useme umekamatiwa Tabora usije kutaja majina yako ukitaja utajua,” ameeleza mahakama akieleza alikaa katika kituo hicho hadi pale alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu tarehe 19/07/2021 lakini aliendelea kukaa na pingu na hazikutolewa.

“Nilipofikishwa mahakamani ndipo nilipokutana na mshitakiwa mwenzangu Mohamed Ling’wenya na wakatufungia selo moja,” ameeleza akiongezabkuwa hakuwahi kuonana uso kwa uso na mshitakiwa huyo tangu walipokamatwa Moshi zaidi ya kuwasiliana kwa njia ya sauti walipokuwa kituo cha Tazara.

Mshitakiwa huyo namba 2 ,Adam Kasekwa ameanza kutoa ushahidi wake kwa upande wa Jamhuri katika shauri dogo baada ya upande wa Jamhuri kuiomba mahakama hii leo kufunga ushahidi wake baada ya mashahidi watatu kati ya saba waliotarajia kuwatumia kutoa ushahidi wao ambapo Wakili wa serikali Mwandamizi aliiomba mahakama kuwaondoa mashahidi wanne waliosalia.

Msingi wa shauri dogo umekuja baada ya upande wa utetezi kutoa mapingamizi mawili kupinga maelezo ya mshtakiwa Adam Hassan Kasekwa kama kielelezo kilichotolewa na shahidi wa kwanza wa kesi ya msingi,ACP Ramadhani Kingai kwa madai kuwa mshtakiwa huyo aliteswa kabla na ya kuchukuliwa maelezo na amedai pia maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria…

Aidha Jaji wa Mahakama Kuu, Mstapha Siyani ameiahirisha Kesi hiyo mpaka terehe 27/09/2021 saa tatu kamili asubuhi ambapo mshitakiwa namba 2,Adam Kasekwa ataendelea kutoa ushahidi wake katika shauri dogo, ambapo pia anatarajiwa kuhuloji upande wa mawakili wa upande wa Jamhuri kisha kuhojiwa tena na Wakili wake (re- examination) kama taratibu za Mahakama zinavyoelekeza.