February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MRITHI WA BENSOUDA ICC AAPISHWA,NI KARIM KHAN

KARIM KHAN

Mwanasheria Karim Khan, ameapishwa rasmi kuwa mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).Khan ambae ni raia wa Uingereza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mgambia,Fatou Bensouda aliyemaliza kandarasi yake ya miaka minane katika mahakama hiyo.

Sherehe za kumuapisha Khan zimefanyika leo Jumatano,June 16 katika makao makuu ya mahakama hiyo yaliyopo The Hague,nchini Uholanzi.

‘‘Niwahakikishie nyote kuwa  nitatekeleza majukumu yangu kikamilifu na nitaitumikia nafasi hii kama mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hii kwa heshima,uaminifu,bila upendeleo,na kwa uangalifu mkubwa’’ amesema Khan katika hafla ya kuapishwa kwake.

FATOU BENSOUDA

Khan anakwenda kuanza kazi katika muda ambao mtangulizi wake  alikuwa anakabiliwa na changamoto lukuki za uhalifu ikiwemo uchunguzi wa uhalifu unaofanywa kwa mamlaka za Palestina,Afghanistan,Myanmar Pamoja na Ufilipino.

Kabla ya uapisho,Khan ambae ni mbombezi wa sheria dhidi ya uhalifu wa kimataifa pamoja na haki za binadamu alichaguliwa kushika wadhifa huo mnamo mwezi Februari.

Kwa muda wa miongo kadhaa,mwanasheria huyo amesimamia kesi katika mahakama zote muhimu na kujijengea heshima kubwa,pia ameshiriki katika sakata nzito ikiwemo uchunguzi maalumu uliofanywa na Umoja wa mataifa juu ya tuhuma zazuhalifu zilizokuwa zinawakabili wanamgambo wa dola la Kiislam (ISS) nchini Iraq.

Baadhi ya kesi maarufu alizosimamia Khan ni pamoja na ile iliyomkabili naibu wa Rais wa Kenya William Rutto katika kesi ya uhalifu dhidi ya Binadamu katika mahakama ya ICC, kesi ya mtoto wa aliyekuwa Rais wa Libya Moammar Gadhafi,pamoja na kesi ya rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor.

Wachambuzi wa masuala ya sheria wanaona mtihani mkubwa alionao Khan kwa sasa ni endapo ataweza kuzishawishi nchi korofi kama Marekani,Urusi,Israel,na China kuwa mwanachama wa mahakama hiyo.

Ikumbukwe pia mtangulizi wake Fatou Bensouda aliwahi kukutana na kigingi cha kuwekewa vikwazo na aliyekuwa rais wa marekani Donald Trump baada ya kuagiza kufanyike uchunguzi dhidi ya madai kuwa vikosi vya Marekani vilikabiliwa na kosa la uhalifu wa kivita nchini Afghanistan.