February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MPANJU AZINDUA RIPOTI YA KIKAO CHA 3 CHA HALI YA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA.

Na Leonard Mapuli,Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba  na Sheria, Amon Mpanju,amefungua rasmi kikao cha kujadili ripoti ya tatu ya mapitio ya hali ya Haki za Binadamu (UPR) kwa  mwaka 2021,kilichoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),kwa mashirikiano na Kituo cha Msaada wa Sheria na  Haki za Binadamu (LHRC),na shirika la Save the Children.

Akimkaribisha mgeni Rasmi,Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania,Onesmo Olengurumwa,amesema Mtandao huo umekuwa ukiratibu  ufuatiliaji na tathmini ya  Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (UPR) kwa niaba ya Watetezi wa haki za binadamu zaidi ya 200 Tanzania bara na Zanzibar.

“Mchakato huu unaendeshwa na serikali za Umoja wa Mataifa kuhakiki hali ya Haki za Binadamu kwa nchi zote ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa,ili kuboresha hali ya Haki za Binadamu katika nchi zote wanachama na kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu ili kuifanya dunia kuwa sehemu salama kwa kila binadamu”,amefafanua Olengurumwa.

Naibu Katibu Mkuu(WKS) Amon Mpanju,akiteta jambo na Mratibu wa THRDC Taifa,Onesmo Olengurumwa.

Kwa upande wake,naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria,Amon Mpanju,amewakikishia wanachama wote wa Mtandao huo,pamoja na wadau kuwa,maoni yote yaliyowasilishwa serikalini yatafanyiwa kazi kwa mujibu Katibu,Mila na desturi,huku akiupongeza Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu,na Asasi zingine za Kiraia, kwa kuwa karibu na serikali na kutoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa haki kwa makundi yote ya binadamu nchini.

“Asasi za Kiraia ni mkono wa kuume wa Serikali,maana zinafika hata tusikofika,na hivyo kutusaidia kwa kiasi kikubwa kuyafahamu mahitaji ya watu,katika eneo hili la Haki za Binadamu”,amesema Amon Mpanju.

Muwakilishi wa LHRC,Raymond Kanegene (Wa kwanza kushoto),na Muwakilishi wa Save the Childeren, Wilbard Muchunguzi (Wa pili Kulia) wakiwa pamoja na Mgeni Rasmi,Amon Mpanju (Katikati).

Katika kikao hicho cha siku moja,kinachofanyika jijini Dar es Salaam,mashirika mengine yaliyoshiriki katika uandaaji,yamewakilishwa na Raymond Kanegene,kwa niaba ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania  (LHRC),huku Shirika la Save the Children likiwakilishwa na Wilbard Mchunguzi.

Mwaka 2021, Tanzania imefanya mapitio ya 3 ya hali ya haki za binadamu (UPR) mnamo mwezi Novemba ambapo ilipokea jumla ya mapendekezo 252 kutoka nchi mbalimbali,na kati yake,ni  mapendekezo 108 tu kati ya 252 (43%) serikali,mengine 12 (4.8%) yakiahidiwa kuzingatiwa,na mapendekezo 132 (52%) hayakukubaliwa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mtandao huo,kiwango cha kukubalika kwa Mapendekezo yanayolewa na nchi wanachama juu ya sheria mbalimbali zinazokiuka Haki za binadamu,unazidi kupungua  kwa serikali ya Tanzania, kutoka 70% (2011), 58%( 2016) hadi kufikia 43% mwaka huu, 2021.