March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MONGELA AIBUA TENA SAKATA LA MGOGORO WA ARDHI LOLIONDO

Na Loveness Muhagazi

Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela hii leo akiwa katika ziara yake wilayani Loliondo amewaeleza wenyeviti wa vijiji pamoja na madiwani mkoani humo, juu ya hatua ya serikali ya kuchukua eneo lenye kilomita za mraba 1500 ambazo zimekuwa na mvutano wa muda mrefu kuwa Pori Tengefu la Loliondo na kuliweka chini ya mamlaka ya hifadhi ya wanyamapori Tanzania, Tanzania Wildlife Authority (TAWA).

Eneo hilo muhimu linatajwa kukatwa kutoka katika kilomita za mraba 4000 ardhi halali ya vijiji vinavyojumuisha mji wa Loliondo na eneo la Waso na vijiji vya Oloirien, Ololosokwan, kirtalo, Oloipiri, Maaloni, Olosoitok, Arash, Ormanie na pia , maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakiishi tangu jadi na kufanya shughuli mbali mbali ikiwemo makazi na malisho ya mifugo.

Wananchi wa Loliondo wamepinga hoja ya serikali iliyoeleza kuwa inataka kulifanya eneo hilo kuwa la uhifadhi na kuutaja uamuzi huo kutokuwa shirikishi na kwamba serikali imeamua kulichukua eneo hilo kwa nguvu kwa nia ya kulikabidhi rasmi kwa kampuni ya kiarabu inayofanya shughuli za uwindaji katika eneo hilo inayoitwa Otelo business cooperation (OBC ) ili kuendesha shughuli za uwindaji.

Eneo hilo lenye kilomita za mraba 1500 lililomegwa na serikali linatajwa kuwa eneo muhimu sana kwa jamii ya kifugaji kwani ndipo hujipatia chakula kwa ajili ya mifugo yao na kuzisaidia jamii za kimaasai kuendelea na shughuli zao za kila siku. Eneo la kilometa za mraba 2500 ni dogo sana ukilinganisha na Idadi ya watu ambayo wakazi wa vijiji hivyo ni takribani ni zaidi ya 170,000.

Kwa kipindi cha karibu miaka 30 sasa eneo hilo la Loliondo na Osero lenye kilomita za mraba 1500 limekuwa likijadiliwa na kutaka kumegwa lakini tawala za marais wote kuanzia wa Rais Mwinyi, Mkapa, Kikwete na hata Rais Magufuli wote hawakuweza kulitoa eneo hilo kutokana na hoja za wananchi kushinda mikakati ya kutaka kulichukua eneo hilo na kukabidhi kwa mwekezaji na kuamua kuwaacha wananchi katika eneo lao, na hasa ikikumbukwa Kuwa wakati Mizengo Pinda akiwa Waziri Mkuu alishakwenda Loliondo na kukabidhi waraka uliowahakikishia wananchi wa eneo Hilo Kuwa ardhi yao haitachukuliwa.

Mgogoro huu umedumu kwa miaka sasa ambapo kila mara viongozi wamekuwa wakitoa matamko mbali mbali kuhusiana na eneo hilo kutengwa na kuwa mali ya Hifadhi jambo ambalo limekuwa likileta mgogoro usioisha katika jamii za kifugaji hasa eneo hilo la Loliondo mpaka sasa serikali imewataka wakazi wa maeneo hayo kusubiri utaratibu wa uchukuliwaji wa ardhi hiyo utakaotolewa na serikali hivi karibuni.