March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MKUTANO WA RAIS,CHADEMA KULETA MARIDHIANO YA KITAIFA?

Na Evarist Mapesa
Miaka nane imepita tangu viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania kukutana na kufanya mazungumzo ya maridhiano katika harakati za kunusuru mchakato wa katiba mpya chini ya Utawala wa Rais mstaafu wa Awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete.
Tangu mwaka huo hadi hivi sasa, hakuna kiongozi yeyote wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyeenda Ikulu kuonana na Rais kwa ajili ya maridhiano licha ya baadhi ya viongozi wa chama hicho mara kadhaa kunukuliwa na vyombo vya habari wakiomba nafasi ya Majadiliano na Rais Lakini shauku na ndoto ya viongozi wa Chadema, kuonana na kujadiliana mambo mbalimbali waliyokuwa wakitamani kuyawasilisha kwa Kiongozi Mkuu wa Nchi sasa imeanza kuonekana tangu March 04,2022 baada ya mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Tangu Rais Samia na Mbowe walivyokutana miezi miwili iliyopita, viongozi hao wamekutana tena May 20, 2022 wakiwa na baadhi ya viongozi wengine kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Hatua hiyo iliweza kuibua hisia za wafuatiliaji wa siasa za Tanzania huku maswali baadhi ya watu wakiendelea kujiuliza nini kinachofuata baada ya mazungumzo hayo.
Kikao hicho kina maana gani?
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa hapa nchini Tanzania wanasema kitendo cha Rais Samia kukutana na viongozi wa pande hizo mbili katika meza moja ni katika harakati za kutengeneza amani na ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania Hamduni Maliseli anasema jitihada zinazofanywa na Rais Samia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa linapaswa kuungwa mkono na watu wote katika kuleta amani na ushirikiano.
“Anachojaribu kukifanya Rais sio kutafuta maendeleo ya nchi bali anajaribu kutafuta amani ya nchi baina ya chama kilichopo madarakani na vyama vingine vya upinzani ili kuweza kutengeneza mazingira ya wao kufanya siasa kwa amani na usalama,” alisema Maliseli.
Hata hivyo Kuna uwezekano mkubwa mwaka 2025 Tanzania kuingia katika uchaguzi mkuu huku vyama vyote vinavyofanya siasa zake vikiwa katika hali ya umoja na mshikamano.
“Kuna uwezekano mkubwa tukaingia katika uchaguzi mkuu tukiwa wamoja zaidi, taifa likiwa moja zaidi kutokana na ahadi aliyoahidi kuwa uchaguzi utakuwa wa haki, Jambo linalotakiwa ni kuendelea kumkumbusha,” amesema Maliseli.
Kwanini Chadema imeridhia kufanya Vikao na Rais?
Miaka mitatu imepita tangu Mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha Upinzani nchini Tanzania Chadema , Freeman Mbowe tangu alipopaza sauti yake kwenda kwa ya kuomba Maridhiano ya kitafa aliyoitoa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara)
Katika mwito alioutoa kwa dakika chache alipopewa nafasi na Hayati John Magufuli, Mbowe alieleza umhimu wa kuwepo kwa maridhiano, upendo na mshikamano katika taifa hilo la Afrika ya Mashariki
”Rais una nafasi ya kipekee kuweka historia ya maridhiano katika taifa letu kwani kuna wengine wanalalamika wanaumia. Rais tumia nafasi hii ukaliweke taifa katika hali ya utengamano,” amesema Mbowe.
“Nimekuja kushiriki sherehe za miaka 58 ya Uhuru kama uthibitisho wa ulazima wa kuwepo maridhiano, upendo, mshikamano katika taifa letu. Namuomba Mungu siku ya leo ikafungue milango tuweze kuishi kama taifa linalopendana, tuvumiliane, tukosoane, turuhusu demokrasia.
Hata hivyo mara baada ya kutoka gerezani, Mbowe alieleza mbele ya vyombo vya habari sababu kuu ya kuridhia kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan, huku lengo kuu ikiwa ni kuleta umoja na mshikamano kwa taifa bila kubaguana kwa itikadi za vyama na kuahidi kuendeleza mazungumzo yatakayoleta muafaka wa siasa za Tanzania.
Wanachama chadema watia Neno
Kumekuwa na hisia mseto tangu kufanyika kwa kikao hicho huku baadhi ya wanachama wa Chadema wakionekana kukubaliana na viongozi wao, na wengine wakiwa bado na mashaka juu ya uamuzi huo.
Martine Maranja Masese ambaye ni mwanachama wa Chadema Kupitia katika ukurasa wake wa twitter aliandika kuwa vigezo na masharti vilitakiwa kufuatwa kabla ya kukutana na kuonesha picha.
“ Maamuzi halali ya baraza kuu yanapuuzwa,unaenda Ikulu kumfaidisha Rais kwa Picha,picha anawaonesha Mabeberu kuwa tupo safi ‘shekeri’ zinaingia” aliandika Masese.
“Twende mezani tukiwa na nguvu, siyo wanyonge,tubebe ajenda, tusihutubiwe tu na kuondoka,vigezo na masharti lazima vizingatiwe”aliongeza Masese.
Tangu chama hicho kilipofanya mkutano wake na Rais Samia pamoja na viongozi wa Chama Tawala (CCM), wanachama wa Chadema wanaamini kuwa huo ndiyo mwanzo mzuri wa kuleta maafikiano.
Twaha Mwaipaya, ni Mwanachama wa chama hicho anasema “Tanzania inahitaji siasa safi na kuaminiana, tusiishi kwa shaka, tutafanya kila aina ya upokonyaji” aliandika Mwaipaya kupitia katika ukurasa wake wa twitter.
kipi kilichozungumzwa katika kikao hicho?
Mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyotolewa kutoka pande zote zilizoshiriki mkutano huo,licha ya katibu mkuu wa Chadema kupitia ukurasa wake wa twitter kusema kuwa taarifa Zaidi kuhusu maudhui na mchakato wa mazungumzo itatolewa wakati muafaka