February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MKATABA WA 5 UJENZI WA BOMBA LA HOIMA-TANGA WASAINIWA.

Na Leonard Mapuli,Dar es Salaam.

Marais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Yoweri Kaguta Museveni  wa Uganda wameshuhudia utiwaji saini wa  mkataba  hodhi (Host Governmental  Agreement) kati ya Tanzania na kampuni ya ECOP juu ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Rais, Dar es  Salaam.

Mradi wa ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka  Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani-Tanga nchini Tanzania kwa awali unatarajiwa kuanza kusafirisha mafuta kiasi cha mapipa 1,046 huku lengo kuu likiwa ni kusafirisha mapipa bilioni 6.5 kwa mwaka na utakamilika ifikapo mwaka 2025.

“Mradi huu utagharimu dola za Marekani bilioni 4.16,na utajengwa kwa miaka mitatu,ingawa wajenzi wanasema itachukua miaka minne kupata mafuta”,amefafanua  Medard Kalemani,waziri wa nishati wa Tanzania alipoelezea mwenendo wa mradi huo mbele ya marais Samia na Museveni.

Mradi huo wa kihistoria unatarajiwa kuleta faida nyingi za kiuchumi kwa pande zote ambapo Uganda itanufaika kwa asilimia sitini za mapato na Tanzania asilimia arobaini na kutoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira kwa wananchi katika maeneo ambako bomba litapita.

“Waganda na Watanzania wanafuatilia kwa ukaribu mwenendo wa mradi huu na wapo tayari kuzitumia fursa mbalimbaliza kiuchumi zitakazotokana na mradi huu”,ameongoza Ghatitu Mariagoreth,waziri wa nishati wa Uganda.

Rais Museveni amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea kasi ya maendeleo kwa pande zote mbili na kuimarisha zaidi ustawi wa jamii na kwamba hata kipato kitakachopatikana kitawasaidia wananchi kupata huduma mbalimbali na kuongeza fursa za uzalishaji mali.

“Sasa ukijiuliza utajiri na ajira zinatoka wapi,kwani ajira zinatoka katika bubondo  (Neno la kiganda lenye maana ya sekta)gani?” ameuliza rais Museveni na kuongeza kuwa vyote hivyo vinaweza kupatikana kutokana na uwekezaji katika maeneo mbalimbali akiutaja mradi huo kuwa sehemu ya uwekezaji mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Licha ya faida za kiuchumi, mradi huo unatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Uganda na Tanzania ambao umekuwa wenye afya tangu nchi hizo mbili za ukanda wa Afrika mashariki zipate uhuru na kwamba uhusiano huo ndio chanzo cha Tanzania kukubali bomba hilo kujengwa Tanzania.

“Nchi yetu imeridhia bomba la mafuta kujengwa katika ardhi yetu lakini pia kujengwa bandari ya kupokea mafuta ghafi kule Chongoleani Tanga”,amesema Rais Samia katika hotuba yake baada ya kushudiwa utiaji wa saini.

Mkataba hodhi uliotiwa saini leo (Mei 20) unakuwa mkataba wa tano kusainiwa baada ya mingine minne kusainiwa kwa nyakati mbili tofauti,mkataba wa kwanza (Ushirikiano) kati ya Tanzania na Uganda ulisainiwa mwezi Mei 2017,huku Mkataba hodi kati ya Uganda na ECOP pamoja na  mikataba ya Uenyeji,Ushuru na Usafirishaji, Umiliki wa hisa, ikisainiwa Mwezi Aprili mwaka huu.