February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MHANGA WA UKATILI WA KIJINSIA AELEZA MACHUNGU ALIYOFANYIWA NA MME WAKE

Na Evarist Mapesa,Mwanza

Ripoti  iliyotolewa  Septemba 2021 na Jarida la Afrika kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia Tanzania miongoni mwa wanandoa, ilionyesha kuwa, asilimia 46 ya wanandoa hufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambapo  asilimia 36 walifanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 32 walifanyiwa ukatili wa kisaikolojia na  asilimia 13 walifanyiwa ukatili wa kingono.

Lakini pia takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2021 watu 1 5 131 walifanyiwa ukatili wa kijinsia huku ripoti hiyo ikionyesha ongezeko la mauaji kwa wanawake walio katika ndoa.

Vitendo hivi vimekuwa vikileta athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na mauaji, ulemavu, majeraha na kusababisha kukosekana kwa amani katika ndoa mwishowe ndoa kuvunjika.

Mkazi wa kisesa wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Lusi Maiko ni mhanga wa ukatilia wa kijinsia ambao alikuwa akifanyiwa na mme wake na kumfanya akose amani katika familia yake.

Lusi alisema kuwa kutokana na mazingira na ukabila ulikuwa ukimfanya mme wake kumlazimisha na kufanya fujo kwenye mambo ambayo sio haki kwa upande wake.

” Ukatili niliopitia naweza kusema ni ukatili wa kijinsia kutokana kwa sababu mazingira niliyokuwa naishi na mme wangu yalikuwa ni manyanyaso ya kiwango cha juu,” alisema Lusi.

Anaongeza kuwa kuna wakati ulifika alikuwa akimtafutia sababu ndogo ndogo na kufuata mila za kizamani kumfanyia ukatili hali iliyopelekea kuyumba kwa familia na amani kutoweka.

“Hali hiyo ilipelekea kuyumba kwa familia, amani kukosekana na akianzisha mahojiano yalikuwa yana ambatana na kipigo, Kutolewa nje na kufungiwa milango mpaka muda mwingine siku tatu”.

” Hali hiyo ilipoendelea niliamua kwenda kwa mwenyekiti wa Kijiji lakini bado alikuwa mgumu na mbishi mno kuweza kutii wito huo hadi ikafikia wakati mwenyekiti akawa anampigia simu lakini alikuwa anaishia kusema hayupo, jambo ambalo liliendelea kuvumiliwa kutokana na kufamiana nae hadi kufikia uvumilivu ulipoisha” alisema Lusi.

Mbali na hivyo Lusi alisema mme wake amewai kuivunja Cherehani ya kushonea nguo kwa kuibonda na nyundo hali ambayo ilimfanya kubakia bila Cherehani ambayo alikuwa akitumia kujiingizia kipato cha kila siku kilichokuwa kinamfanya kuendesha familia yake.

Vipigo vya mara kwa mara pamoja na ukatili mwingine aliokuwa akitendewa na mme wake umepelekea madhara katika afya yake ikiwa ni pamoja na mgongo kuuma pindi akiwa katika mzunguko wa siku zake za hedhi.

“Mpaka kufikia saizi nadhani imenisababishia madhara katika mwili wangu kwa sababu hicho kitu hakiwezi kusahaulika kichwani mwangu na inapofikia Mwanamke unaingia kwenye siku zako huwa naumwa mgongo na kunifanya kushindwa kunyenyua hata ndoo ya maji hali ambayo binafsi inanifanya kushindwa kusahau  japo kuwa huwa natumia dawa,” alisema .

Hata hivyo ametoa ushauri kwa jamii kuacha tabia ya kufanya ukatili kwa mtu mwingi kutokana na athari ambazo zinaweza kutokea.

Kutokana na vitendo hivyo Mhadhiri msaidizi katika chuo kikuu cha mtakatifu Augustino SAUT Mwanza kutoka idara ya Sociology Linah Kabula alisema mtu yoyote bila kujali jinsi anaweza kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

“Vitendo atakavyofanyiwa na jinsia njingine ambavyo vita msababishia maumivu iwe ni ya kisaikolojia, kimwili au ambayo yanaweza kudhuru nyanja ya kiuchumi huo tayari unakuwa ni ukatili wa kijinsia” alisema Kabura

Aliongeza kuwa jamii inapaswa kubadilika kutokana na dhana iliyojengeka katika jamii kuwa wanawake na watoto ndio hufanyiwa ukatili wa kijinsia na wanaume hawawezi kufanyiwa ukatili huo.

“Inategemeana kuna wale ambao huwa wanakimbia kutoka kwenye imaya anayokaa, wengine hushirikisha watu au kuripoti kwenye vituo husika kwa mfano kuna madawati ya jinsia ambayo watu wamekuwa wakiogopa kwenda kuripotia unakuta wanawake sana ndio wanaenda hali ambayo imekuwa ikipelekea kushuhudia vifo kutokea”.

“Hatua za kufanya shirikisha watu wakaribu sana wakupe ushauri lakini pia shirikisha vyombo vya usalama ili uweze kusaidiwa” alisema Kabura.

Nae Mtaalamu wa Sheria kutoka shule ya Sheria katika chuo kikuu cha SAUT Mwanza Kalla Frank alisema Sheria za Tanzania zinasema kila mtu ana haki ya kulindwa, kuishi pasipo kunyanyasika.

” Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 13 imeelezea kwa mapana juu ya usawa wa kila mtu mbele ya Sheria ikiwa na maana na kuwa hakuna mtu mwenye Mamlaka ya kumnyanyasa mtu mwingine,” alisema mtaalamu Frank.

Ametoa ushauri kwa jamii na asasi za kiraia kuendelea kutoa elimu kwa wanachi ili kuweza kupunguza matatizo yanayohusiana na matukio ya ukatili katika jamii.