February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MGOGORO NGORONGORO WAZUA MAPYA;MADIWANI WATOA TAMKO

Baraza la Madiwani Wilaya ya Ngorongoro limetoa tamko kuhusiana na mgogoro wa Ngorongoro  na kueleza kuwa ziara ya Waziri mkuu wilayani humo hivi karibuni imezua taharuki kubwa na tishio la upokonywaji wa ardhi bila kuangalia maslahi yao yatakayopotea.

Katika tamko hilo lililotolewa na Baraza hilo juma hili na kusainiwa na madiwani  37 limesema wameshuhudia waandishi wa habari na baadhi ya wawakilishi wa wananchi wakizuiwa kuingia katika mkutano wa wilaya ya ngorongoro hivyo kupelekea taarifa kutoka za upande mmoja tofauti na ilivyokuwa tarafa ya Loliondo.

“Ujio wa Waziri Mkuu tarafa ya ngorongoro ulikuwa tofauti na ule wa Loliondo tulishuhudia watu wakizuiwa na kukaguliwa sana kabla ya kuingia,pia waandishi wa habari wengi walizuiwa kuingia hivyo kufanya taarifa zitoke za upande mmoja tu tofauti na ilivyokuwa Loliondo ambapo maoni ya viongozi yaliwafikikia wale wanaowawakilisha pamoja na alichosema waziri Mkuu”imesema taarifa hiyo.

Aidha Baraza hilo limekemea vikali tabia za ubaguzi dhidi ya jamii hiyo ya kimasai waishio Ngorongoro huku wakieleza kusikitishwa kwao baada ya Waziri Mkuu kushindwa kukemea tabia hiyo hadharani.

“Tulitegemea serikali ingekemea udhalilishwaji tuliofanyiwa kama jamii ya wilaya ya Ngorongoro na vyombo vya habari na baadhi ya wabunge kwa namna ubaguzi wa kikabila tofauti na misingi ya nchi yetu” imesema.

Tamko la Baraza la madiwani Ngorongoro limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutembelea eneo hilo na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa wananchi wa Tarafa ya Loliondo na Ngorongoro kwa nyakati tofauti.wakati wa vikao hivyo Waziri Mkuu aliwaahidi wananchi hao kuwa hakuja na malori kuwaondoa wananchi hao kwa nguvu bali kujadiliana kuhusu namna bora ya kuendeleza uhifadhi na wananchi katika eneo hilo la urithi wa dunia.

Licha ya tamko na ziara hiyo ya Waziri Mkuu madiwani wamedai kuwa hawakubaliani na agizo la kuweka alama Kilomita za mraba 1500 za ushoroba wa wanyama Loliondo.

“Waziri mkuu pia ameagiza maeneo ya kilomita za mraba 1500 yaanze kuwekwa vijialama, hili limezua taharuki kwani inaashiria kuanza kwa zoezi la kugawa ardh ya vijiji,hili kama viongozi wa wananchi hatukubalini,”

Aidha wameongeza kuwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wanategemea mifugo ili kuweza kuendesha familia zao na kama mipango ya serikali ikipita itawafanya kuwa masikini.

“Mipango ya serikali ikipita mifugo haitapata tena malisho na maji,watu watakuwa masikini na wakimbizi wa ndani na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji itaongezeka,” imeeleza taarifa hiyo