March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MGOGORO NGORONGORO: VYOMBO VYA HABARI VITOE TAARIFA SAHIHI

Katika tamko liliotolewa hapo jana na wanawake wa jamii ya kimasai waishio Ngorongoro wamekana kupewa fedha au hongo ya aina yoyote ili wakatae pendekezo la serikali la kuhama katika hifadhi ya Ngorongoro ili kupisha uhifadhi.

Wanawake hao wamelaani propaganda zinazoendeshwa mitandaoni na baadhi ya watu,wanahabari na baadhi ya vyombo vya habari kwa nia ya kuichafua jamii hiyo ili waonekane ni adui wa uhifadhi katika hifadhi ya Ngorongoro.

Hii si mara ya kwanza kwa vikundi vya jamii ya kimasai kutoka hadharani na kukanusha taarifa zinazozagaa dhidi yao zikidai kuwa wanakosa maisha bora,elimu n ahata kuishi katika umasikini uliokithiri hifadhini humo na wakati mwingine propaganda hizo zilifika mbali Zaidi na kusema kuwa kama jamii hiyo ikiendelea kuishi hifadhini hapo basi kwa miaka ijayo uhifadhi utapotea.

Waswahili husema mkono mtupu haulambwi tunadhani ni vyema wanaosambaza taarifa za uhifadhi kutoweka wangekuja na tafiti za kisayansi zinazoonesha hali ilivyokuwa miaka 60 iliyopita kabla ya jamii hiyo kuingia Ngorongoro,hali ilivyo sasa na miaka ijayo.
Sipingani na hoja ya kuimarisha uhifadhi lakini napendekeza majadiliano huru yanayolenga kuonyesha namna uhifadhi ulivyoathiriwa au kunufaishwa na uwepo wa binadamu katika hifadhi ya Ngorongoro lakini pia utalii ambao Taifa lianingiza mamilioni ya fedha kupitia hifadhi ya Ngorongoro.Je uwepo wa jamii ya kimasai umenufaisha au kuharibu shughuli za kitalii?

Miongoni mwa malengo ya Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro ni kukuza na kuimarisha jamii ya asili ya kimaasai inayoishi hifadhini,kama uhifadhi na shughuli za kibinadamu zimeshindikana katika eneo la Ngorongoro,NCAA itoe ufafanuzi wa kina kwanini imeshindwa kutekeleza majukumu yake.

Kumeshuhudiwa taarifa mbalimbali zinazotolewa katika mitandao na watu mbalimbali ikiwemo wanahabari n ahata vyombo vya habari ambao kazi yao kuu ni kusimamia katika misingi ya kitaluma ya kuipa taarifa yoyote mizania sawa baina ya wanaotuhumiwa na wanaotuhumu, taarifa zingine zimekwenda mbali Zaidi na kuandika Asasi za kiraia zinatoa fedha kushawishi wananchi wagome kuhama hifadhini na zingine kudai baadhi ya viongozi wa Asasi zhizo wamekimbilia mataifa ya nje taarifa ambazo hazina uthibitisho wala hazikuhoji wanaodaiwa kukimbia sababu ya kuondoka kwao kama kweli wamekimbia nchi kisa Ngorongoro.

Serikali kupitia Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa wakati akiwa ziarani Wilayani Ngorongoro Februari mwaka huu alisema serikali haina nia ya kuwahamisha wakazi hao kutoka Ngorongoro na wala hakwenda na malori ya kuwahamisha kama wengi walivyodhani na kuwataka wakazi hao kusikiliza serikali na sio wenye lengo la kuichonganisha serikali na wananchi.Waziri Mkuu alisema pia katika mkutano huo Tarafa ya Loliondo kuwa amefika ili wajadiliane namna bora ya uhifadhi.

Lakini licha ya kauli hiyo ya Waziri Mkuu iliyoleta faraja baada ya taharuki nzito kwa wananchi hao bado kumeendelea kuwepo kwa propaganda hasi na maneno yanayolenga kuwachonganisha wananchi na serikali,wanaosambaza taarifa hizo wametumwa na nani? Au wanafanya hivyo kwa minajili gani na nani yupo nyuma yao?

Taarifa mbalimbali zinazotolewa sio tu zinalenga kutoa taharuki bali kupakaza matope taassisi ama watetezi wa haki za binadamu ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wananchi wa Ngorongoro,wengi wakiambiwa wamekuwa vibaraka wa mataifa ya nje yenye upinzani wa kitalii na Tanzania huku wengine wakielezwa kukimbia nchi na kufadhili wananchi wa Ngorongoro ili wasihame hifadhini.

Je kupaza sauti dhidi ya jamii yoyote inayokumbwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ni kosa la uhaini? Ama ni kinyume cha sharia? Kama wapo wanaotetea uhifadhi kwa kuchafua wengine bila kuchukuliwa hatua za kisheria basi wawepo na wanaoteta wananchi bila kubughudhiwa au kuonekana vibaraka wa mabeberu.

Hoja zipingwe kwa hoja, utetezi unaolenga kuchafua watu wengine ama jamii zingine ili kuifanya hja yako iwe ya uzito haina misingi ya kibinadamu na inalenga kuminya haki za binadamu wengine.

Nadhani wadau wa uhifadhi,jamii na vyombo vya habari vitoe taarifa sahihi kuhusu mgogoro wa Ngorongoro na kuacha watazamaji na wafuatiliaji wa haki za binadamu kuung’amua ukweli,visitoe taarifa za habari za mezani (kupika) na zifanye mahojiano na wakazi halisi wa eneo la Ngorongoro na sio kueneza propaganda zinazoeneza chuki dhidi ya jamii hiyo.

MAKALA HII NI MAONI BINAFSI YA MWANDISHI KUHUSU MTAZAMO WAKE JUU YA MGOGORO WA NGORONGORO