February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MGOGORO NGORONGORO: KAMATI MAALUM YA KURATIBU MAPENDEKEZO YA WANANCHI YAUNDWA,KUWASILISHWA KWA VIONGOZI WA JUU WA SERIKALI

Wananchi wa wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wameunda Kamati maalum itakayoratibu mapendekezo ya wananchi kuhusu mgogoro wa ardhi unaoendelea katika tarafa ya Ngorongoro na Loliondo.Kamati hiyo ya watu 60 inayowajumuisha wawakilishi wa Madiwani, wawakilishi wa wenyeviti, wawakilishi wa kinamama, wawakilishi wa viongozi wa kimila na baadhi ya wasomi     wa jamii hiyo ya kifugaji.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamati hiyo hii leo na kutiliwa saini na Mwenyekiti wa Viongozi wa Kimila Wilayani Ngorongoro,Melau Oleshaudo imesema Kamati hiyo itakuwa ni kiungo kikubwa kati ya wananchi na serikali katika kuelekea kwenye hatua za wali za utatuzi wa mgogoro huo baina ya pande hizo mbili.

“Kazi kubwa ya kamati hii yenye mchanganyiko wa makundi ya kijamii ni kuwa kiungo kikubwa kati ya wananchi na serikali katika kuelekea kutatua migogoro hii bila kuadhiri pande zote mbili zinazovutana. Kamati hii imeanza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kwa vijjji vyote vinavyozunguka eneo lenye mgogoro wa kilimeta za mraba 1500 pamoja na vijjji vyote vya Tarafa ya Ngorongoro,”imeeleza.

Wanawake wa jamii ya kimasai kutoka katika Wilaya ya Ngorongoro wakiwa na mabango ya kuashiria kutokuwa tayari kuhamishwa kutoka Ngorongoro

Aidha taarifa hiyo imeongeza tayari wameanza kukusanya maoni kutoka kwa wananchi pamoja na vijiji vinavyozunguka eneo lenye mgogoro la Kilometa za mraba 1500 pamoja na vijiji vyote vya tarafa ya Ngorongoro na ndani ya wiki moja Kamati hiyo itawasilisha mapendekezo yake kwa viongozi wa juu wa serikali na kwa umma.

“Baada ya kuona mchakato wa kuwashirikisha wananchi na makundi ya jamii kuwa hafifu katika kutatua migogoro hii, tumeona ni muda muafaka sasa kujitafutia njia ambayo mapendekezo yetu kama jamii yanaweza fikia wahusika na umma wa Watanzania kwa ujumla,”imesema.

Pia Kamati hiyo imesema  inaendelea na kazi ya kuratibu na kuchakata maoni ya wananchi ili kuandaa taarifa moja ya Wilaya hiyo ambayo inajumuisha mapendekezo kuhusu mgogoro wa Hifadhi ya Ngorongoro na wa Loliondo.

Wajumbe wa Kamati Maalum wakiwa katika Mkutano wa Kuratibu mapendekezo ya wananchi

“Wakati tunaendelea na uratibu huu wa maoni tunaishauri serikali isitishe mikakati yoyote inayoendelea Ngorongoro na Loliondo kwa sasa ili tupate nafasi ya kuja kupata meza ya mazungumzo badaye. Wakati huo huo tunashauri mchakato wa watu wa kuhama kwa hiari usitumike kama silaha ya kugawa jamii ya wanangorongoro,”ameongeza

Aidha Kamati hiyo maalum imempongeza Rais Samia Suluhu kwa kufanya mabadiliko ya mawaziri katika Wizara ya Maliasili na Utalii na kutoa wito kwa Waziri wa Maliasili na Utalii aliyeapishwa hivi karibuni,Pindi Chana kuanza na suala la mgogoro wa Ngorongoro kwa kuzuia propaganda dhidi ya wananchi hao hasa jamii ya kimasai na kusitisha mipango yote inayoendelea kwa kutoa nafasi ya kusikiliza wananchi.

“Waziri akataze matisho na kamatakamata yoyote dhidi ya wanajamii, viongozi na watetezi wa haki za binadamu wanaosimama kutetea haki za jamii, kuzuia vitisho dhidi ya waandishi wanaotoa taarifa za umma, tatu kuzuia Wanangorongoro kuitwa si Watanzania, nne kuagiza huduma za msingi ziendelee kutolewa kwa wananchi wa tarafa ya Ngorongoro, tano akutane na kamati hii ili kuanza kujenga mikakati ya pamoja,” ameongeza Oleshaudo katika taarifa iliyotolewa leo

Kamati hiyo maalum imeundwa ikiwa ni jitihada za wananchi hao kutafuta suluhu ya kudumu katika mgogoro huo wa ardhi katika tarafa tatu za Wilaya ya Norongoro na katika uundaji wa Kamati hiyo wameongozwa na viongozi wa Wilaya pamoja na Mbunge wa Wilaya ya Ngorongoro.

o