February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MFUMUKO WA BEI: SERIKALI KUPUNGUZA KODI BIDHAA MUHIMU

Serikali ya Tanzania, imesema itashusha viwango vya kodi katika bidhaa muhimu, ili kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi,  uliosababishwa na mfumuko wa bei.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Waziri huyo wa fedha, amesema suala hilo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuchukua hatua za muda mfupi katika kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa  bei ya bidhaa muhimu kwenye soko la dunia, iliyosababishwa na mgogoro wa kivita kati ya Urusi na Ukraine.

“Bidhaa ambazo zinanunuliwa na zinasafirishwa, jitihada tunazifanya za kupunguza makali, madhara yatakuwepo sababu ni jambo la dunia nzima, tukisema tusione haya madhara, tutatengeneza madhara,” amesema Dk. Mwigulu.

Dk. Mwigulu amesema, Serikali itapunguza kiwango cha kodi ya sukari inayoingizwa nchini kutoka nje ya nchi, ambapo punguzo hilo halitakuwa chini ya asilimia 10.

“Sukari itakayoingia tutapunguza rate (kiasi) yake ya kodi, kwa kiwango ambacho hakitakuwa chini ya asilimia 10. Baada ya hapo Juni tutaangalia trend (mwenendo) inasemaje, tutakapopitisha sheria ya kodi tutakuwa tumesoma mambo yanaendaje tutapitisha hatua gani tunazochukua,” amesema Dk. Mwigulu.

Dk. Mwigulu amesema, Serikali itapunguza kodi inayotozwa kwenye mafuta ya petroli na dizeli.

“Kwenye mafuta ya magari ambayo ndiyo injini katika shughuli za uzalishaji, Rais ameelekeza, tutaangalia tena gharama zile ambazo sisi Serikali zinatuhusu, tutaangalia tuone kiwango tutakachopunguza, tunaamini tutapunguza mzigo kwa wananchi,” amesema Dk. Mwigulu.

Aidha, Dk. Mwigulu amesema timu ya wataalamu ya Serikali, itaketi  ndani ya wiki moja, kuangalia namna ya kupunguza tozo za mafuta, ili kudhibiti mfumuko wa bei ya bidhaa.

“Kwenye mafuta tutaangalia tuone kiwango ambacho tutapunguza, uamuzi wa Rais ni wa busara kwamba maeneo ya shughuli za uzalishaji ziendele. Lakini gharama za matumizi ya kawaida, timu yetu ya watalaamu itakaa ndani ya wiki moja, watakuwa wamejua hatua zipi tuchukue,” amesema Dk. Mwigulu.