March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MFUMO JINAI KUFUMULIWA, ADHABU MBADALA ZAJA

Serikali  ya Tanzania, iko mbioni kuufumua mfumo wa jinai ili kuuboresha ikiwemo kwa kuanzisha adhabu mbadala kwa ajili ya kupunguza msongamano wa mahabusu.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, akijibu swali la Mbunge Viti Maalum, Felista Njau, aliyehoji kwa nini Serikali isianzishe utaratibu wa vifungo vya nje kwa makosa madogo ili kupunguza msongamano huo.

“Wakati tunapitisha bajeti ya wizara mwaka huu, tulisema moja kati ya vipaumbele ni kwenda kuuangalia upya, kuufumua na kuupanga mfumo wa jinai hapa nchini. Katika mpango huo, moja kati ya jambo hili ni kuangalia adhabu mbadala ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu katika magereza,” amesema Dk. Ndumbaro.

Katika hatua nyingine, Dk. Ndumbaro amesema zoezi la upangaji anuani za Makazi pamoja na utoaji vitambulisho vya taifa vinavyotolewa na NIDA, likikamilika, watuhumiwa wataanza kujidhamini wenyewe ili kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani.