February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MCHUNGAJI ATAKA “KUVUNJIKA KWA NDOA” KUTANGAZWA JANGA LA KITAIFA.

Mch.Enock Mlyuka-Mkurugenzi TaMCare.Picha:Hilder Ngatunga.

Na Leonard Mapuli (lennymapuli@gmail.com)

  • Ni baada ya Kukithiri kwa visa hivyo
  • Asema hakuna tofauti na Majanga mengine kama Corona
  • Adai kuvunjika kwa ndoa kunaua,na kusababisha uharibifu na upotevu wa mali kama majanga mengine.

Mchungaji wa Kanisa la K.K.K.T ambae pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Marriage and Child Care (TaMCare),Dkt Enock Mlyuka,ameiomba serikali kutangaza tatizo la “Kuvunjika kwa Ndoa”  kuwa Janga la Kitaifa  kama yalivyo Majanga mengine yanayotambuliwa duniani ikiwemo Corona,Njaa,Mafuriko,Matetemeko na mengineyo yanayosababisha maafa, uharibifu na upotevu wa  mali.Mchungaji huyo ameongeza kuwa,kuvunjika kwa ndoa kunasababisha maafa kwa baadhi ya wanaondoa kufa ama kuuana,pamoja na uharibifu wa mali ikiwemo kuchoma moto na kuharibu mali baada ya ndoa kuvunjika.

Mchungaji huyo ameongeza,kuwa,katika kazi zake za kiroho za kila siku,kuvunjika kwa ndoa ndilo tatizo kubwa analokutana nalo kila siku katika majukumu yake ya “kuchunga kondoo”Ina kuongeza kuwa Kondoo walio kwenye ndoa (Wanandoa)ndio wanaoongoza kupotea kwa ndoa kuvunjika

Ameyasema hayo katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania,(THRDC) kuwawezesha baadhi ya wanachama wake kuzifahamu  sheria,sera na miongozo ya kukabiliana na majanga pamoja na kuzuia maafa, inayofanyika jijini Dar es Salaam

Onesmo Olengurumwa-Mratibu THRDC.(Picha:Hilder Ngatunga).

Awali akifungua Warsha hiyo,Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu,Onesmo Olengurumwa, amesema suala la majanga halina mwenyewe kwa kuwa mengi hutokea ghafla na mengine hayawezi kuzuilika,ikiwemo Moto,Mafuriko,matetemeko,Magonjwa,na vimbunga kwa kutaja baadhi na hivyo kuwataka Watetezi wa Haki za binadamu kuwa mabalozi wa kutoa elimu na hasa kwa majanga yanayoweza kuzuilika badala ya kuiachia serikali pekee kutekeleza jukumu hilo.

“Muda mwingine,watu wanaamini suala la uokoaji ama kukabiliana na majanga ni kazi ya serikali,hii siyo sahihi,ni kazi ya kila mtu tukiwemo sisi Watetezi wa Haki za Binadamu”,amesema Onesmo Olengurumwa na kukazia zaidi  suala la wananchi kupatiwa elimu na kujengewa uwezo wa kuelewa kuwa suala la kupambana na majanga ni la kila mtu.

Olengurumwa pia amelalamikia uwekezaji mdogo  wa wadau na serikali katika kuzuia majanga mbalimbali na kuwekeza nguvu kubwa  kwenye kukabiliana na matokeo yanayotokana na majanga ikiwemo maafa na  uharibifu,ambapo ameiomba ofisi ya Waziri Mkuu kuwekeza zaidi katika kutoa elimu ya kujikinga na kuyakabili majanga, pamoja na kuwa na sera shirikishi kwa wadau na wananchi kwa ujumla ili kuepusha gharama zinazoweza kujitokeza kutokana na majanga ikiwemo maafa.

Kanali Jimmy Said-Mkurugrnzi Idara ya Maafa-O.W.M.(Picha:Rodrick Mushi).

Mgeni Rasmi katika warsha hiyo, Kanali Jimmy Said,ambae ni Mkurugenzi wa Idara ya Kukabiliana na Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,amesema kukosekana kwa elimu ya kukabiliana ama kuzuia majanga kumeendelea kuwa ni wakala mkubwa wa madhara makubwa yatokanayo na majanga katika jamii nyingi ikiwemo maafa.

“Tukiwekeza zaidi katika kutoa elimu ya kuzuia majanga,tutapunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa majanga,kuliko kusubiri kukabiliana,maana kukabiliana na janga lolote ni gharama zaidi ambapo kama lingezuiwa (Kwa majanga yanayozuilika)basi lisingeleta hasara”,amesema Kanali Jimmy na kurejea uwepo wa janga la Uviko-19,linaloweza kuzuilika kwa kufuata miongozo inayotolewa na Wizara ya afya ikiwemo kuvaa barakoa,kunawa mikono kwa maji tiririka,matumizi ya vitakasa mikono,na kujiepusha na misongamano ya watu ili kuzuia maambukizi ya virusi hivyo, kuliko kukabiliana navyo kwa mashine za kusaidia kupumua ambazo ni gharama kubwa.

Aidha Kanali Said amesisitiza watu kutumia taarifa za kisayansi zaidi za kuzuia ama kukabiliana na janga la Corona, ikiwemo  kupata  chanjo ambayo tayari imeanza kutolewa kote nchini,na kupuuza maneno yanayotolewa na watu ambao si wataalamu wa afya za binadamu,wala utafiti wakiwemo viongozi wa dini wanaoshawishi waumini wao kutopatiwa chanjo kwa kuwaaminisha kuwa chanjo hiyo ina madhara siku za usoni kwa wote wataopatiwa.

“Chanjo ya Corona si suala la kiroho ,ni la Sayansi”,ameongeza Kanali Jimmy.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,ambayo ndiyo yenye mamlaka kisheria juu ya kupambana na kuzuia majanga,serikali inaandaa Mkakati wa kuzuia na kupambana na maafa unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni kusaidia jamii ya Watanzania kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali yanayoikumba Tanzania na kusababisha maafa.

Janga la Corona bado limesalia kuwa janga la juu zaidi nchini Tanzania kwa sasa ambapo juhudi kadhaa zinaendelea kuchukuliwa ili kukabiliana nalo.Majanga mengine yanayotikisa nchini  ni Moto,Umasikini,Ukosefu wa ajira,Ukimwi,na endapo ombi la mchungaji Erick la serikali kutangaza  uvunjifu wa ndoa kuwa janga,itaongeza idadi ya majanga yanayoikumba Tanzania kwa sasa.