February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MBUNGE MADAMA ALIA NA KILIMO CHA TIJA, AMPA KIBARUA WAZIRI

Mbunge wa Madaba,Dkt Joseph Mhagama ameishauri serikali kutafuta mbinu za kutatua changamoto za mitaji ili mkulima aweze kupata zana bora za kilimo pamoja na kuongeza mtaji wa Benki ya Kilimo ili Tanzania iwe na kilimo chenye tija.

Mbunge huyo amesema hayo wakati akichangia Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni hapo jana, ameongeza kuwa Benki ya Kilimo iliyotazamiwa kutatua changamoto za kilimo nayo inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo kuwa na mtaji mdogo kuweza kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.

“Mtaji mzima wa TADB ninaambiwa kama nimekosea mtanirekebisha ni Bilioni 268 na kama asilimia 60 ya watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo inamaanisha kama kila mtanzania atakopa kwaajili ya kilimo kutoka benki hii atapata sh. 7000 tu”amesema Dkt Joseph Mhagama.

Aidha amempongeza waziri wa kilimo kwa kuweza kuongeza zaidi Bilioni 600 katika Bajeti ya kilimo jambo ambalo halijawahi kuwepo miaka ya nyuma.

Aidha amempa kibarua Waziri wa Kilimo kuweza kutafuta fedha za kuongeza mtaji wa Benki ya Kilimo ili kutatua changamoto ya tija katika kilimo

Pia ameainisha kuwa sera ya mikopo katika Benki ya Kilimo ni miongoni mwa changamoto katika sekta hiyo ambayo amesema sera hiyo ya mikopo inafanana na benki za kibiashara katika utekelezaji wake.

“Benki hii haikukusudiwa iwe benki ya biashara za kawaida ilikusudiwa iwe benki ya uwekezaji na kama ningeruhusiwa kubadilisha jina na kupendekeza jina ningependekeza iitwe Tanzania Agricultural Investment Bank” akiongeza kuwa mikopo inayotolewa na Benki hiyo ni ya muda mfupi itayomwezesha mkulima kununua mazao leo na kuuza kesho.

Kwa upande mwingine Dkt Joseph Mhagama amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya nchini,pia amepongeza uandishi wa Bajeti Kuu ya serikali ya mwaka 2022/2023 kuwa ni wa kipekee na unaojibu hoja za wananchi wa Tanzania.