February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MBUNGE CCM AWAKEMEA WANAOMNANGA HAYATI MAGUFULI

MBUNGE wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde, amewataka watu wanaomsema vibaya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli, waache kwani haiwasaidii kitu kwa kuwa amefariki dunia.

Lusinde anayefahamika kwa jina maarufu la Kibajaji, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, bungeni jijini Dodoma.

“Tusifikiri kumsema vibaya Magufuli kutasaidia, hawezi kujibu. Hayupo, kama una tatizo naye maliza utakuja kukutana naye kwa Mungu. Mtu akishatangulia kitabu chake kinafungwa, tunamuachia Mungu kuja kutoa hukumu,” amesema Lusinde.

Lusinde amesema kuwa, kitendo cha watu kushindwa kukosoa dosari zake anapokuwa madarakani ni uoga, kwani wanapaswa kuzungumza wakati akiwa madarakani.

“Inakuwaje watu mnakuwa waoga, viongozi wakiwepo hamsemi, wakiondoka mnasema. Huu ni uoga uliopitiliza. Mtu mmoja tu (Lazaro Nyalandu) alisema kwa vitendo yeye hawezi kufanya kazi na Magufuli, aliacha ubunge hapa akaondoka, wote tuliobaki hapa ni wa Magufuli,” amesema Lusinde.

Mbunge huyo wa Mvumi, amedai watu wanaomsema vibaya Magufuli aliyefariki dunia akiwa madarakani tarehe 17 Machi 2021, watakuja kufanya jambo hilo kwa mrithi wake, Rais Samia Suluhu Hassan, atakapong’atuka madarakani.

“Na mheshimiwa Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) ndiyo kazi tunayofanya(kumsifu). Tusiwe wanafiki hawa watu sasa hivi wanamsema vibaya Magufuli na kumsifu Rais Samia ni wanafiki siku Samia akiondoka watamsema vibaya hivyo hivyo ni bora mimi Lusinde ambaye niko wazi na siwezi kuacha,” amesema Lusinde.

Aidha, Lusinde amemtaka Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliombe radhi Taifa na familia ya Magufuli, kwa kumnanga hadharani.

“Zitto aelewe kwamba, suala la kufiwa ni suala kubwa. Anatutaka tunayempenda Magufuli tukazikwe naye, anatulazimisha tumseme vibaya Maalim Seif hatuwezi. Kusema wanaompenda Magufuli wakazikwe na Magufuli maana yake nini? Hii ni kashfa kubwa sana Zitto aombe radhi asirudie tena,” amesema Lusinde.