February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MBUNGE ATAKA MIKATABA MIBOVU YA UWEKEZAJI IPELEKWE BUNGENI

Mbunge  wa Kisesa, Luhaga Mpina, ameshauri mikataba mibovu ya uwekezaji iliyoingiwa kati ya Serikali na watu binafsi, ipelekwe bungeni kwa ajili ya kujadiliwa kwa kuwa inaliingizia taifa hasara.

Ushauri huo wa Mpina umetolewa leo Jumatatu, bungeni jijini Dodoma, akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.

Baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha wa 2020/21, kubaini Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC), nchini Uingereza, imeiamuru Serikali kuilipa mabilioni ya fedha Kampuni ya Symbion Power, baada ya kuvunja mkataba wake na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

“Wabunge tukataeni mikataba ya aina hii, tukatae kulipa hizi fedha na uchunguzi ufanyike, ukaguzi wa kina ufanyike kile kilichojificha nyuma ya Symbioni tuweze kuyajua yote na tuweze kujua haki zetu zilizokuwepo, lakini miktaba hii ambayo tunaitambulisha ni mibovu, iitishwe hapa bungeni tuweze kuifuta,” amesema Mpina.