February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MBUNGE ALILIA MATIBABU BURE KWA WATU WENYE ULEMAVU

Mbunge wa  Viti Maalumu, Stella Ikupa, ameiomba Serikali iweke utaratibu maalumu wa kutoa matibabu bure kwa watu wenye ulemavu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama hizo.

Ikupa ametoa ombi hilo leo Jumanne, bungeni jijini Dodoma, akichangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.

Mbunge huyo viti maalumu kundi la watu wenye ulemavu, amesema walemavu wanakabiliwa na ukosefu wa huduma za matibabu, kwa kuwa wengi wao wanaishi kwenye kipato cha chini.

“ Niombe Serikali iweze kufanya zoezi lililofanyika kwa wazee, kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wale ambao hawana uwezo wa kupata matibabu, ili basi vitambulisho vile viwawezeshe kutibiwa kwa urahisi,” amesema Ikupa.

Katika hatua nyingine, Ikupa ameiomba Serikali izisimamie halmashauri zote nchini, ili ziweze kutoa mafuta kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino).

“Changamoto ya utolewaji mafuta ya watu wenye ualbino kwenye halmshauri zetu imekuwa ya muda mrefu, miongozo ipo, kanuni zinaongea wazi lakini suala hili halitekelezeki kwenye halmashari zetu, nimekuwa nikipokea simu kutoka kwa watu wenye ulemavu wakilalamikia suala hili, kwamba halmashauri hazito mafuta,” amesema Ikupa na kuongeza:

“Niiombe Serikali suala hili liweze kutekelezwa kwa maana ya kwamba halmashauri ziweze kutenga kununua na kusambaza mafuta haya kwa watu wenye ualbino.”