February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MBARONI TUHUMA ZA MAUAJI YA KINYAMA MTOTO WA MDOGO WAKE

LATIFA Bakari (33), mkazi wa Mabibo, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kumuuwa mtoto wa mdogo wake, mwenye umri wa miaka miwili na miezi minne.

Akielezea tukio hilo, leo Jumanne, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, ACP Jumanne Muliro, amedai Latifa alitekeleza tukio hilo tarehe 5 Aprili 2022, baada ya kumpiga kupita kiasi mtoto huyo aliyekabidhiwa kwa ajili ya kumlea.

“Tarehe 6 Aprili 2022, aliuchukua mwili wa mtoto, kuukunja, kuuweka kwenye ndoo ya plastiki kisha kuudumbukiza kwenye kiroba na kwenda kuutupa eneo la River Side Ubungo. Baada ya majirani kutomuona mtoto huyo kama ambavyo si kawaida walitoa taarifa Polisi,” amesema Kamanda Muliro na kuongeza:

Kamanda Muliro amesema “Polisi ilimuhoji kwa kina mtuhumiwa akakiri mauaji hayo na kwenda kuwaonesha Polisi mwili wa mtoto huyo ulipokuwa. Mwili huo umepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi na mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya mifumo ya kisheria kukamilika.”

Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amesema wanawashikilia watu wanne, kwa tuhuma za kujaribu kuhujumu miundombinu ya Shirika la Umeme Tanesco ikiwemo Nyaya aina ya Copper kwa lengo la kuziuza.

Watuhumiwa hao ni, Omary Ally, Juma Sulleiman, Amos John na Makolo Machage, walikamatwa tarehe 10 Aprili 2022 na kwamba walipohojiwa na kupekuliwa walikutwa na viroba vinne vya nyaya za shaba zilizochunwa.