February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAZUNGUMZO YA RAIS SAMIA NA TUNDU LISSU YAIBUA GUMZO NCHINI TANZANIA

Na: Anthony Rwekaza

Kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Februari 16, 2022 kutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu mjini Brussels Nchini Ubelgiji wanasiasa pamoja na wadau wanaofatilia siasa za Tanzania wameibua mijadala yenye mtazamo tofauti juu ya makutano hayo.

Mazungumzo hayo amabayo yamefanyika kufuatia Rais Samia kukubali maombi yaliyowasilishwa na Lissu kumuomba kukutana na kuzungumza kuhusu masuala mbalimbali yanayoigusa Tanzania hususani uwanda wa siasa.

Muda mchache mara baada ya taarifa ya kukutana kwao kuanza kuenea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hususani baada ya taarifa rasmi kutolewa kwa umma kupitia kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Ikulu, wadau ambao ni watumiaji wa mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, Instagram pamoja na JamiiForums walianza kutoa maoni yao juu ya tendo hilo ambalo alikutegemewa na watu wengi.

Wengi wao wameonekana kutoa maoni yenye kuwapongenza kwa hatua hiyo, hasa wakielekea pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kwenye ziara ya kikazi Nchini Ubelgiji mara baada ya kumaliza ziara yake Nchini Ufaransa, wakidai ameonesha ukomavu wa kisiasa.

Kwa upande wake mwanasiasa ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema Chama chao kimekuwa kikisisitiza juu ya mazungumzo ambayo yanaweza kupelekea ufumbuzi wa tofauti za kisiasa katika kuleta mabadiliko, hivyo amempongeza hatua ya Rais kukubali ombi la kuonana na Lissu.

“Hatimaye hekima imetawala na mlango wa mazungumzo umefunguka. Sisi ACT wazalendo tokea awali tunasisitiza kwamba mazungumzo ndiyo njia sahihi ya kupata ufumbuzi wa tofauti zetu za kisiasa na kuleta Mabadiliko. Hatua ya Rais kukubali kuonana na Bwana Lissu ni ya kupongeza sana” Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Pia Wanasiasa wengine ambao wamewai kuwa wabunge kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Godbless Lema na Peter Msigwa wameguswa na kitendo hicho na kudai kuwa Rais kukutana na Lissu ni jambo jema kwa kuwa wamekuwa Chadema wakiomba mazungumzo na Rais kwa muda mrefu.

Pia Mwanaharakati ambaye ni mwandishi wa maandiko ya kisiasa na kijamii, Mwanachama wa CCM Tadei Ole Mushi kupitia ukurasa wake wa Facebook amesema alichokifanya Lissu akikindhani na ombi alilolitoa Zitto Kabwe mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan alipomtaka kutumia mamlaka yake kumwachia Freeman Mbowe, licha ya alichodai kuwa Zitto alishambuliwa sana baada ya kuwasilisha hoja hiyo kwa Rais Samia.

“Sioni tofauti yoyote ya alichokiongea Zito siku aliyomuomba Mama Samia kumwachia Mbowe na hiki Lisu alichokiongea Jana. Tulimshambulia sana Zitto lakini nakumbuka niliandika hapa kuwa iwe iwavyo na kwa njia yoyote ile Mbowe tunamhitaji na Familia yake inamhitaji sana awe HURU. Wote wanaomba hii Kesi iishe na Mbowe awe Huru. Wote hawataki hii Kesi iende kwenye hatua za Mwisho za Hukumu.” Mwanachama wa CCM, Tadei Ole Mushi

Aidha Tundu Lissu ameeleza baadhi ya mambo ambayo amepata fursa ya kumueleza Rais Samia Suluhu Hassan katika mazungumzo waliyofanya, ameeleza kuwa kati ya mambo hayo ni juu ya kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambapo amedai amemuomba Rais kutumia mamlaka yake ili kuhakikisha kesi dhidi ya Mbowe inaodolewa Mahakamani huku akidai kuwa amemueleza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hawasaidii CCM, Chadema bali inamuumiza Mbowe, amedai kuwa Rais Samia amemuaidi kushughulikia.

“Nimemuambia Rais Samia kwamba kesi ya Mbowe haikisaidii Chama chake Rais (CCM), haikisaidii Chama chetu (CHADEMA), inamuumiza Mwenyekiti wetu Mbowe na Chama chake, inawauemuambia Rais afanye analoweza kufanya kwa mamlaka yake kama Rais ahakikishe hii kesi ya Mbowe inaondolewa Mahakamani, hakuna sababu yoyote ya kuendelea na kesi ambayo kila Mtu anaona na ushahidi unaonesha Mahakamani kwamba ni mambo ya kuungaunga tu na Rais Samia ameahidi kwamba atalishughulikia” Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu

Ameongeza kuwa amemueleza Rais Samia kuwa anaitaji kurudi Tanzania, hivyo amedai amemuomba atoe kauli ya kumkaribisha nyumbani na kumtoa wasiwasi juu ya usalama wake mara baada ya kurejea, huku pia amedai a Rais Samia amekubali kumsaidia kupata hati ya kusafiria (passport) kutokana na aliyokuwa nayo awali kudai kuwa ilibiwa akiwa Nchini Ujerumani Mwezi Januari.

“Nimemuambia Rais Samia nahitaji kurudi nyumbani na kwasababu ya mazingira niliyoondokea nyumbani nimemuomba yeye kama Rais atoe kauli ya kunikaribisha nyumbani na kunitoa wasiwasi kwamba nikirudi nyumbani nitakuwa salama na Mh. Rais amesema hilo atalifanyia kazi. Rais Samia amekubali pia kuhakikisha napata hati ya kusafiria kwasababu passport yangu iliibiwa mwezi uliopita nikiwa Ujerumani”Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu

Vilevile Lissu amesema ameongea na Rais Samia kwa niaba ya Godbless Lema na Wenje ambao nao wapo uhamishoni Nchini Canada kwa madai ya kuhofia usalama wao, kuwa amemuambia kama ilivyo kwake na hao walikimbia Nchi kwasababu ya vitisho dhidi ya maisha yao, hivyo amedai kuomba kuhakikishiwa usalama wao ili wapate uhakika kwamba vitisho hvyo havitakuwepo.

Itakumbukuwa Tundu Lissu Mwaka 2017 alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, ililazimika Chama chake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kumsafirisha kumpeleka Nairobi kwa Ndege kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, kabla ya badae baada ya kufanyiwa upasuaji kadhaa kupelekwa Nchini Ubelgiji kwa ajili ya upasuaji mwingine kwa kuondoa baadhi ya vipande vya risasi vilivyodaiwa kusala kwenye mwili wake.

Tundu Lissu alivuliwa Ubunge rasmi kwa madai kuwa halikosa kuwasilisha taarifa rasmi kwa kukosa baadhi ya mikutano ambayo kisheria upelekea Mbunge kupoteza sifa za Ubunge, kufuatia jambo hilo wanasisiasa pamoja na baadhi wanaharakati walionesha kutokubaliana na hatua hiyo.

Kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja Tundu Lissu amekuwa mkosoaji wa Serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Kikwete alifanya hivyo akiwa Mbunge kwa tiketi ya Chadema, alikuwa mkosoaji kwenye Serikali ya awamu ya Tano iliyoongozwa na Hayati Rais Magufuli pia amekuwa mkosoaji kwenye Serikali ya awamu ya sita inayongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan licha ya kuwa nje ya Nchi mara baada ya uchaguzi Mkuu 2020, ambapo alikuwa mgombea Urais kupitia tiketi ya Chadema ambapo alishika nafasi ya pili kwenye kinyanganyiro.

Lissu kipindi akipatiwa matibabu Nchini Kenya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania alifika hospitalini kumuona na kumjulia hali alipokuwa amelazwa, hatua hiyo ilipongezwa na wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kisiasa Nchini Tanzania hata nje ya mipaka ya Nchi hiyo.

Lakini Tundu Lissu anayeishi Nchini Ubelgiji kwa madai ya kuhofia usalama wake, ambapo kwa mara kadhaa amekuwa akieleza juu ya kutokuwepo kwa taarifa ya uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwake, anadai amekuwa akidai kuwa anayo hofu kulejea tena Nchini kwa kuwa waliomshambulia bado hawajulikani, lakini Jeshi la Polisi limewai kusikika kuwa hawajalifumbia macho tukio hilo na usalama upo kwa kila raia hata kwa Tundu Lissu kama akiamua kurejea kama ilivokuwa kwenye kipindi cha uchaguzi aliporejea kwa ajili ya shughuli za uchaguzi.

Hata hvyo Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema yeye pamoja na Chama chake akiwemo Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe ambaye anakabiliwa na kesi yenye mashtaka ya ugaidi pamoja na viongozi wengine wa chama wamekuwa wakiueleza umma juu ya ombi la kutaka kukutana na Rais Samia Suluhu ili kujadili musuala mbalimbali yanayogusa siasa za Tanzania, ambapo waliweka wazi kuwa wameshamwandikia barua ya kutaka kuonana nae.