February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAUAJI YA MTOTO MWENYE UALBINO TABORA, LHRC WAJA JUU

Kituo cha sheria na Haki za Binadamu LHRC, kwa kushirikiana na shirika la Tabora Vision Community (TAVICO) kimelaani tukio la mauwaji lililogharimu uhai wa mtoto anayekadiriwa Kuwa na umri Kati ya miaka 5 hadi 6 yaliyotokea Kati ya tarehe 3 au 4, mwezi Mei mwaka huu.

Wa mujibu wa Taarifa, mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuukuta Mwili huo ukiwa umekatwa mikono yote miwili, macho yote mawili yakiwa yameng’olewa, sikio la kushoto likiwa limekatwa, na sehemu zote za Siri zikiwa zimeondolewa.

Mwili mtoto huyo uliokotwa na wanakijiji ukiwa umetelekezwa katika majani, katika eneo la shamba karibu na dimbwi la maji katika kitongoji Cha Usadala, kijiji cha Utemini, kata ya Ndono, wilaya ya Uyui, mkoa wa Tabora.

Mpaka sasa mtoto familia ya marehemu haijapatikana, huku Mtendaji wa kata akidhihirisha Kuwa ndani ya vijiji 8 vya kata hiyo hapakuwepo na familia yoyote iliyopoteza mtoto, na Kuwa huenda tukio Hilo likawa limetendeka mbali na hapo kuja kutupa Mwili huo katika kijiji hicho kwani hakuna kuashiria chochote cha purukushani katika eneo alipotupwa mtoto huyo.

Kufuatia tukio Hilo kituo cha Sheria ana Haki za Binadamu, LHRC kimeshangazwa na kitendo cha Jeshi la polisi kukaa kimya bila kutoa Taarifa za wazi kwa Uma juu ya kitendo hicho cha kikatili, na kwamba kitendo hicho kinapelekea Wadau na Watetezi wa haki za Binadamu kutilia mashaka utashi wa mamlaka hizo.

“Kitendo cha Mamlaka ya mkoa wa Tabora kunyamazia kimya unyama huu kinatutia mashaka kama Wadau wa masuala ya Haki za Binadamu, juu ya utashi wa mamlaka hizo kwenye ulinzi wa haki za Binadamu na Utawala bora” LHRC katika tamko

Kituo cha sheria na Haki za Binadamu LHRC kimetoa Rai kwa serikali kuhakikisha Taarifa za tukio Hilo zinawekwa wazi kwa umma na kuonyesha njia ambayo inaweza kutumiwa na wazazi au walezi kupata Taarifa sahihi za alipozikwa Ndugu yao, lakini pia kufanya upelelezi wa kina na kubaini wahusika na kuwachukulia hatua stahiki.