March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAREKEBISHO SHERIA: WADAU WATAKA POLISI WASIFANYE MSAKO BILA KIBALI CHA MAHAKAMA

JUKWAA la Wahariri Tanzania, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wameshauri Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015, ifanyiwe marekebisho ili kuondoa kifungu kinachoruhusu Jeshi la Polisi, kufanya upekuzi kwa mtuhumiwa bila ya kibali cha mahakama.
Ushauri huo umetolewa leo Alhamisi, katika mafunzo ya sheria za habari Tanzani kwa wanahabari, yaliyofanyika mtandaoni.
Akizungumza katika mkutano huo, Wakili James Marenga, amesema mahakama ndiyo chombo pekee chenye kutoa maamuzi, hivyo Polisi wanatakiwa kwenda kuomba kibali cha kufanya upekuzi kwa mtuhumiwa wa makosa ya mtandao.
“Katika sheria hii tunasema Polisi inapewa mamlaka haya, bado mahakama ipewe nafasi sababu katiba inasema mahakama ndiyo chombo pekee ndiyo chenye mamlaka ya kutoa uamuzi juu ya suala fulani, Polisi waende mahakama kama wanataka kuchukua vifaa vya mtuhumiwa, Waende mahakama kupata oda na si vinginevyo,” amesema Wakili Marenga.
alisema ina mapungufu hususani katika kifungu chake cha nne, kinachoelekeza mtu kukutwa na hatia iwapo itabainika alitenda kosa kwa kudhamiria.
“Karibu vifungu ambavyo nimeonesha, ikiwemo namba nne inatumia neno kudhamiria, kesi nyingi zinashindwa mahakamani kwa kuwa huwezi kuiona dhamira,” alisema Marenga.
Mbali na kifungu hicho, Marenga alisema, kifungu cha 17, 18 na 22, vinatumia neno ‘si chini ya’, kitendo ambacho kinaweza kuifungua mlango kwa wale wanaotoa maamuzi ikiwemo majaji na mahakimu kuweka adhabu kubwa kulingana na mshtakiwa husika.
“Tanzania ina sheria nyingine zinazosimamia amsuala ya adhabu na sheria imetoa maelekezo ya ukomo wa adhabu, unapotumia maneno si chini ya, maana yake unatoa nafasi ya mtoa maamuzi aweze kutoa dhabu isiyotakiwa, inaweza kupitiliza kiwango,” alisema Marenga.
Wakili huyo alisema, kifungu cha 30 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao, kinahitaji marekebisho kwani hakibainishi mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi zinazohusu masuala ya mtandao.