February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAMBO MATANO KUTIKISA BARAZA KUU LA CHADEMA

Mkurugenzi  wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, amesema ajenda tano zitajadiliwa katika Baraza Kuu la chama hicho, linalotarajiwa kuketi Jumatano, tarehe 11 Mei 2022, kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mrema ametoa taarifa hiyo leo Jumatatu, akitangaza ratiba ya vikao vikubwa vya Chadema, kwa wanahabari jijini Dar es Salaam.

Ajenda ya kwanza iliyotajwa na Mrema ambayo itajadiliwa na wajumbe wa baraza hilo, ni mpango mkakati wa miaka mitano na mpango kazi wa mwaka wa Chadema.

“Na kwenye mpango mkakati wa miaka mitano maana yake tunakwenda kukubaliana tunaanzaje kuanzia sasa mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Tunakwendaje kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024. Na hii ni baada ya baraza kupokea taarifa ya uchaguzi mkuu wa 2020,” amesema Mrema.

Mrema amesema ajenda ya pili itakuwa ni ratiba ya uchaguzi wa ndani wa Chadema, huku nyingine ikiwa ni rufaa ya nidhamu iliyokatwa na waliokuwa wanachama wake 19, wanaopinga kuvuliwa uanachama kwa tuhuma za usaliti baada ya kuapishwa kuwa wabunge viti maalumu, kinyume na msimamo wa chama hicho.

“Ajenda nyingine ni rufaa ya nidhamu, hapa ndilo lile eneo ambalo waandishi wengi mnapenda kutuulizia, tuna waliokuwa wanachama wetu 19 ambao walishafukuzwa na kamati kuu, ambao wamekata rufaa Baraza Kuu,” amesema Mrema.

Mrema amesema “wameshaitwa kwa barua rasmi, wamepelekewa wito wote wameshaupata kwa ajili ya kuja kusikiliza rufaa zao, kwa hiyo kama wasipkuja rufaa zitatolewa uamuzi.”

Wanachama hao ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), Halima Mdee. Nusrat Hanje (aliyekuwa Katibu wa BAVICHA). Hawa Mwaifunga, Jesca Kishoa na Agnesta Lambart.

Mrema amesema ajenda nyingine itakayojadiliwa na baraza hilo, ni mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu uliosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta.

“Ajenda nyingine itakayojadiliwa na Baraza Kuu, itakuwa taarifa ya Kamati Kuu kuhusu kupanda kwa gharama za mafuta kulikopelekea gharama za maisha kuwa ngumu. Baraza litajadili tutatoka na njia tunashauri hatua gani zichukuliwe kwa dharura ili kukabiliana na hali hii,” amesema Mrema.