February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI KESI YA KUPINGA MASHARTI YA VIGOGO KUSHTAKIWA

Na: Anthony Rwekaza

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Dar es Salaam Jumanne Feburuari 15, 2021 imetoa hukumu ya kesi namba 09/2021 iliyofunguliwa na Mtetezi wa Haki za Binadamu ambaye ni Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Uamuzi wa ya Kesi ambayo ilikuwa ikipinga marekebisho ya Kifungu namba 4 (2,3,4 na 5) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi Sura ya 3. Marekebisho yaliyotungwa mwaka 2020 na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetolewa mbele ya jopo la majaji watatu, Jaji Elinaza Luvanda Jaji Joseph Mlyambina na Jaji Stephen Mrimi Magoiga katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

Katika uamuzi uliotolewa ni kwamba Kifungu namba 4 (2) (3) (4) (5) cha Sheria ya
utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi Sura ya 3, ni sahihi na kuwa kifungu hicho hakikiuki Ibara ya 26(2) na 30(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mahakama imesema Kifungu hicho (Kifungu cha 4 (2) (3) (4) (5) kinakidhi vigezo vya kikatiba na vya mikataba mbalimbali ya
kimataifa.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mlyambina,
amesema kuwa kifungu hicho hakipo kinyume na Katiba, hivyo mahakama imefikia uamuzi wa kutupilia mbali kesi hiyo,ambapo imetoa sababu za kufikia uamuzi huo kuwa ni kutokana na takwa la kuonesha namna
ambayo mtu ameathirika yeye binafsi kabla ya kufungua kesi kama ilivyo kwenye kifungu cha 4 (2,3,4,5) ambalo ni takwa la kikatiba kwenye Ibara ya 26(2).

Pia sababu nyingine ambayo imeelezwa na Mahakama ni kuwa hitaji la kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwaniaba ya viongozi wakuu wa mihimili ya nchi kuwa mamlaka hayo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yapo kikatiba.

Katika Marekebisho hayo ambayo yalipelekea kufunguliwa kwa shauri namba 9/2021 yanamtaka mtu ili aweze kufungua kesi anapaswa kuonesha namna ambayo yeye binafsi ameathirika.

Wakili Olengurumwa alidai kuwa kifungu hicho kinakiuka Katiba ya Tanzania, misingi ya mgawanyo wa madaraka, utawala wa sheria na utawala bora kama inavyoelekezwa na matakwa ya Katiba hiyo.

Alidai kifungu hicho kinakiuka mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania iliingia ikiwemo mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa.

Pia Olengurumwa katika kesi hiyo alidai kuwa kifungu hicho kimempa mamlaka makubwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kinyume na Katiba.

Aidha akizungumza mara baada ya kutolewa hukumu hiyo, Wakili wa THRDC, Paul Kisabo kwa niamba ya waleta mashtaka amedai kuwa mahakama imetoa uamuzi huo lakini kwa upande wao hawajaridhishwa na uamuzi huo hivyo wanakusudia kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania muda wowote kuanzia ulipotolewa uamuzi huo ambao wameonesha kutorizika nao.

Itakumbukuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Marekebisho ya Sheria (Na. 3) ya mwaka 2020. Kufuatia marekebisho hayo Wakili Onesmo Olengurumwa alifungua shauri akidai kuwa marekebisho hayo kimsingi yanaweza kuondoa au kufuta ufunguaji wa kesi zenye maslahi kwa umma Nchini Tanzania.

Pia Baadhi ya wanaharakati pamoja na taasisi mbalimbali za kutetea masuala ya haki za binadamu walionekan kuikosoa sheria hiyo, itakumbukwa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walipinga muswada wa sheria wa marekebiaho ya sheria mbalimbali nchini namba 3 wa mwaka 2020.

THRDC na LHRC kwa pamoja walitoa tamko la kupinga muswada huo Alhamisi Juni 4, 2020 mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa alisema katika mswada huo kuna marekebisho ya Sheria ya utekelezaji wa Haki za Kimsingi na Wajibu ya 1994 (BRADEA).

Olengurumwa kwa alisema, marekebisho ya kifungu Kifungu namba 4 cha BRADEA kilirekebishwa na kusomeka kwamba, maombi ya kufungua kesi Mahakama Kuu hayatakubaliwa endapo hayajaambatanishwa na kiapo cha mlalamikaji kuelezea jinsi alivyoathiriwa na uvunjifu wa haki na wajibu katika ibara ya 12 hadi 29 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

Aliongeza kuwa Kifungu namba 7(4), ikiwa malalamiko ya uvunjifu wa haki unaelekezwa kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania au, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, au Jaji Mkuu wa Tanzania, malalamiko hayo yatafungliwa dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali ikiwa na maana hakutakuwa na uwezekano wa kufungua kesi dhidi ya viongozi hao.

Pia katika mkutano huo na wanahabari kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Anna Henga alisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya utekelezaji wa haki za msingi na wajibu yanapingana na ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Baada ya Tanzania kujitoa kwenye mahakama ya Afrika sasa Azaki hatuwezi kwenda huko sasa hata kwenye mahakama za ndani hatutaweza kwasababu sheria hii inaweza kuzuia haki hiyo,” amesema.

Hata hivyo, Henga alisema marekebisho hayo aliyaona kama ni muendelezo wa kutaka kunyima haki, alisema hivyo huku akidai kuwa hata sababu za Tanzania kujitoa katika mahakama ya Afrika hazijulikani.