February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAHAKAMA YAKATAA KUPOKEA MAELEZO YA VIDEO YA MKE WA BILIONEA MSUYA

Na: Anthony Rwekaza

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeikataa kielezo ambacho kina kipande cha video (clip) ya maelezo ya mshitakiwa Miriam Mrita, ambaye ni mke wa bilione Erasto Msuya kufuatia ukiukwaji wa matakwa ya sheria ya inayoelekeza namna ya kuwasilisha kielelezo hicho mahakamani hapo.

Uamuzi huo umetolewa March 8, 2022 Jaji Edwin Kakolaki, ambapo alisema kati ya hoja tano anakubaliana na hoja moja na pingamizi zilizotolewa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuwa kielelezo hicho kilichokuwa kinaombwa kupokelewa mahakamani hapo hakikuwahi kuorodheshwa wala kusomwa katika hati ya uhamishaji wa kesi hiyo kutoka mahakama ya chini kwenda Mahakama Kuu kama sheria inavyotaka.

Pia Jaji alisema kuwa upande wa mashtaka ulikiuka kifungu cha 246 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai CPA kutokana na kushindwa kuorodhesha kielelezo katika nyaraka ambazo zilitakiwa kwenda kutolewa mahakamani.

Aliongeza kuwa hoja ya upande wa mashtaka ilieleza kuwa walizingatia kifungu hicho kwani mahakama na washitakiwa walifahamishwa kuhusu kielelezo kinachoombwa kutolewa kwamba ni sehemu ya kielelezo halisi.

Lakini pia ilielezwa kuwa kilitajwa wakati wa usikilizwaji wa awali na imeongelewa kwenye maelezo ya shahidi namba sita ambaye alieleza namna alivyopata kielelezo hicho.

Hata hivyo Jaji aliesema kuwa ni takwa la kisheria kifungu cha 246 kifungu kidogo cha pili cha CPA, nyaraka yoyote ya ushahidi inayotakiwa kutumika mahakamani kwa upande wa mashitaka ni lazima iorodheshwe na isomwe kwa washitakiwa katika hatua ya ‘Commital’ na kutofanya hivyo kunaweza kupelekea kielelezo hicho kutopokelewe mahakamani.

Aliendelea kusema kifungu hicho kinamaanisha pale mshitakiwa atakapofikishwa katika mahakama ya chini, atasomewa mashitaka yaliyopelekwa mahakama Kuu na kufafanuliwa mashitaka hayo kwa sababu maelezo yake yanatakiwa kusomwa na kuelezwa kwa kuwa yana ushahidi ndani yake yanayokusudiwa kutumiwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kama kielelezo.

Alisema mahakama hiyo ilijiuliza kama kielelezo hicho ni sahihi kwa mujibu wa kifungu namba 3(1) cha sheria ya Ushahidi ambayo inaeleza kuwa nyaraka inayokuwa ndani ya kompyuta na kitu ambacho kinaweza kutunzwa kwa ajili ya matumizi ya baadae, kusomwa au kuangaliwa kinaweza kuwa nyaraka na kama inabishaniwa kitapaswa kuwa na kigezo.

Aliafanua kuwa mahakama hiyo iliona kuwa kielelezo hicho ambacho ni ‘min video tape’ ni nyaraka kama zilivyo nyaraka nyingine, hivyo ilitakiwa kusomwa na kuorodheshwa kwenye mahakama za chini kama sheria inavyotaka.

Aliendelea kusema kuwa kuhusu kusoma maelezo ya shahidi na kutajwa kwa kielelezo hicho pekee haikuwa inajitosheleza kwa kuwa kielelezo hicho kilipaswa kuorodheshwa na kusomwa mahakamani hapo.

Alifafanua kuwa htaji la kuorodheshwa na kusomwa kwa kielelezo ni lazima kwa sababu linatoa uhakika kwa mshitakiwa na kumpa haki ya usawa na si kupokea ushahidi wa kushtukizwa.

Jaji aliesema kuwa Mshitakiwa anapaswa kujua undani wa ushahidi uliotolewa juu yake ili kumsaidia kujua kwenye uandaaji wa ushahidi wa wake wakati wa Mahakama itakapo mpa nafasi ya kujitetea.

Alisema kuwa mahakama hiyo haikubaliani na hoja za upande wa mashitaka kuwa waliorodhesha ‘mintap video’ kama nyaraka, hivyo haiwezi kuchukuliwa kuwa kielelezo halisi na hakuna inakosa uwezekano wa kuwa ushahidi halali wa kielektroniki halali.

Uamuzi huo ulikuja kufuatia upande wa mashitaka katika kesi hiyo kupitia kwa shahidi wao wa sita, Mkaguzi wa Polisi (Inspekta), Alistides Kasigwa, Afsa kutoka Makao Makuu ya Jeshi ya Polisi, Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi kuieleza mahakama kuwa alimrekodi mshitakiwa huyo wakati akitoa maelezo yake mbele ya askari Inspekta Ratifa katika kituo kidogo cha Polisi Uwanja wa Ndege, Dar es Salaam, mnamo Agosti 8, 2016.

Mbali na Mrita, mshitakiwa mwengine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Revocatus Muyela (40) ambao wanadaiwa kuhusika na mauaji ya Aneth Msuya ambaye ni Dada wa bilionea Erasto Msuya kwa kukusudia.

Mauaji hayo yalidaiwa kutendeka Mei 25, 2016, maeneo ya Kibada Kigamboni Jijini Dar es Salaam, hali ambayo iliibua sintofahamu mpaka kufunguliwa kwa kesi hiyo.