February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAHAKAMA YAIPA JAMHURI SIKU NNE KUWASILISHA HATI KINZANI KESI YA TITO

Na Mwandishi wetu

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Dar es Salaam, imetoa siku nne kwa upande wa Jamhuri kuwasilisha hati kinzani katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mtetezi wa haki za binadamu na mwanaharakati  Tito Magoti na mwenzake wakipinga mahabusu kunyimwa haki ya kupiga kura wakati wa uchaguzi.

Amri hiyo imetolewa tarehe 7 Machi 2022  mbele ya Jaji John Mgetta baada ya upande wa Jmhuri kuomba kupewa muda, wakati kesi ilipokuwa inatajwa mahakamani hapo ambapo .Upande wa Jamhuri umeamriwa kuwasilisha hati kinzani kwa maandishi  tarehe 11 Machi 2022, kisha upande wa wadai utaijibu tarehe 18 Machi mwaka huu, wakati kesi hiyo itakapotajwa.

Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nalindwa Sekimanga, Emmanuel Kawishe, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Inspekta wa Polisi kutoka Jeshi la Magereza nchini, Zabron Simion na upande wa wadai ukiwakilishwa na Wakili John Seka na Paul Kisabo.

Tito na mwenzake, John Tulla, wamefungua kesi hiyo namba 3/2022, dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Jeshi la Magereza mnamo tarehe 28 Februari 2022, Tito anaiomba mahakama itoe amri kwa NEC na wenzake wanaoshitakiwa katika kesi hiyo , ilimpe fidia kwa kushindwa kumuwekea mazingira yeye na mahabusu wenzake, kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Wapeleka maombi wamedai kuwa, NEC imepewa mamlaka chini ya Ibara ya 5 (1) ya Katiba, kuhakikisha kila raia mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, anayekidhi vigezo kwa kushiriki uchaguzi, anapewa haki ya kupiga kura katika uchaguzi hivyo NEC ilikiuka misingi ya katiba katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, kwa kutowaandikisha mahabusu walioko magereza wakisubiri usikilizwaji wa kesi zao, kwenye daftari la wapiga kura .

Hivyo wanaiomba mahakama itamke kuwa, masharti ya kifungu cha 11 (1) (C), cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, hayaendani na matakwa ya kifungu cha 5 (2) (C) cha katiba pia wafungwa wanaotumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita, kuwa wanastahiki na wana haki ya kuandikishwa kama wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura, kalba ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.