March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAHAKAMA YAAGIZA MBOWE AACHIWE,UPANDE WA MASHITAKA WAAGIZA VIELELEZO VIRUDISHWE

Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi, Dar es Salaam, imewaachilia huru Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu,kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka yaliyokuwa yanawakabili.

Amri hiyo imetolewa na mahakama hiyo leo Ijumaa, tarehe 4 Machi,2022 naJaji Joachim Tiganga siku ambayi upande wa washitakiwa walitarajiwa kuanza kutoa utetezi wao na kwakuwa hawakuwepo mahakamani hivyo mahakama inaandaa amri ili watolewe katika mahabusu za magereza waliyopo.

“Baada ya mahakama kusikiliza hoja iliyoletwa na mawakili wa Serikali ikieleza mahakama kwamba DPP chini ya kifungu cha  91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, hana nia ya kuendelea na shauri kwa sababu hiyo shauri liondolewe.  Mahakama ikauliza upande wa pili na katika mazingira hayo mahakama inasema shauri hili namba 16/2021 la uhujumu uchumi lililokuwa linawakabili  washtakiwa wote wanne limeondolewa,”Jaji Tiganga.

Pia Jaji Tiganga ameagiza upande wa mashtaka kurudisha vielelezo vya washtakiwa vilivyochukuliwa kwa ajili ya ushahidi.

“Kwa sababu kuna vielelezo vilitolewa mahakamani, virudishwe na upande wa mashtaka sababu maombi yameondolewa bila washtakiwa kuwepo, mahakama inaanda amri kusudi magereza walipo washtakiwa waachiwe mara moja leo si zaidi ya hapo,” amesema Jaji Tiganga.

Mbali na Mbowe, wengine waliokuwa wanashtakiwa katika kesi hiyo iliyokuwa namashtaka ya ugaidi matano, ni Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.