February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI YAIAMURU TANZANIA IREKEBISHE SHERIA YA VYAMA VYA SIASA

Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), imeiamuru Serikali ya Tanzania kurekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa, ili iondoe vifungu vinavyokiuka mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, katika hukumu ya kesi namba 3/2020, iliyofunguliwa na wanasiasa wa upinzani, akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kupinga sheria hiyo wakidai inampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Wengine waliofungua keai hiyo ni, Hayati Maalim Seif Shariff Hamad. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe. Mwenyekiti wa Chama cha CHAUMMA, Hashim Rungwe na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC).

Hukumu hiyo ya EACJ, imesema sheria hiyo inakiuka vifungu vya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sehemu ya 6d , 72.

Katika kesi hiyo, kina Mbowe walikuwa wanapinga vipengele  vya sheria ya vyama vya siasa, ikiwemo  kifungu kinachompa Msajili wa vyama vya siasa, mamlaka ya kuingilia wakati wowote shughuli za chama cha siasa.

Vifungu vingine vilivyopingwa ni kile  kinachompa msajili wa vyama vya siasa,  mamlaka ya kuingilia uongozi wa chama cha siasa na kumsimamisha uanachama mwanachama yeyote kushiriki shughuli za kisiasa.

Walidai Vifungu vyote hivyo  vinakiuka misingi ya utawala bora na  kidemokrasia, pamoja  na    mkataba wa EAC.