February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

MADEREVA BAJAJI WENYE ULEMAVU WAFIKISHA KILIO KWA RC DAR

Na Mwandishi wetu

Madereva wa bajaji wenye ulemavu, wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, awapige marufuku madereva wasiokuwa na ulemavu, kuingia katikati ya jiji hilo wakidai wanawaharibia biashara zao.

Kilio hicho kimetolewa leo Jumanne na madereva hao waliandamana kutoka Kituo cha Feri, kilichopo Posta, hadi ofisini kwa Makala, Ilala jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kufikisha kilio chao.

Ramdhani Hussein, amesema ili wao waondokane na changamoto ya umasikini na kuombaomba inabidi watengenezewe mazingira mazuri ya kufanya kazi wanazoziweza, hususan ya kuendesha bajaji.

Amesema na wao wanatamani watekeleze majukumu ya ujenzi wa taifa lao ikiwemo kulea familia zao kama wanavyofanya watu wengine wasiokuwa na ulemavu.

“Tunataka ifike mahalala mwanangu anasoma kwenye shule ambayo mwanangu anasoma na mtoto wa afisa polisi. Ndiyo tunavyotaka, sisi sio wa kwenda kuomba. Lakini tutayapataje haya? Tutayapata pale ambapo tu haki itafanyika ya kuondoa watu wasio na ulemavu mjini na kuacha watu wenye ulemavu,” amesema Hussein.

Hussein amesema “na sisi sio kwamba tunasema kwa bahati mbaya, tuna sababu. Niwaambieni ukimkuta mlemavu anatambaa kama mimi yuko kwenye boda huyo kimbia atakuwa ni jini. Hawezi kukaa kwenye boda, ukimkuta mlemavu nimebeba zege kichwani kimbia huyo sio mtu ni majini ya baharini.”

Hussein amesema, walemavu hawawezi kufanya kazi nyingi kama inayokuwa kwa watu wasiokuwa na ulemavu.

‘Ukimkuta mlemavu yuko barabarani anatembeza nguo za mitumba, muangalie vizuri huyo mlemavu wa aina gani sababu hatuwezi hivyo vitu. Kazi yetu tuliyoiweza ni moja ya kuendesha bajaji humu katikati ya mji. Hao wenzetu wana uwezo wa kufanya chochote,” amesema Hussein.

Naye Rashid Champunga, amesema madereva wa bajaji wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa abiria kutokana na kuporwa abiria na madereva wasiokuwa na ulemavu.

Amesema, kitendo hicho kinawakosesha fedha za kukidhi mahitaji yao na kulipa marejesho ya mikopo waliyochukua.

“Ambao sio walemavu wanachukua abiria, inafikia hatua tunapigwa. Juzi mmoja alipigwa katika purukushani za kugombea abiria. Serikali inatuweka kundi gani na ukiangalia bajaji zetu za mikopo hadi matajiri wanafikia hatua ya kutunyang’anya bajaji zao wakijua tunapata hela tunafanya starehe,” amesema Champunga.

Akijibu malalamiko hayo kwa niaba ya Makala, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigijia, amesema wanafanyia kazi malalamiko hayo, huku akiahidi yatapata ufumbuzi kabla ya tarehe 1 Aprili mwaka huu.

Ludigija amesema Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, imetenga vituo viwili katikati ya mji kwa ajili yao, huku wasio na ulemavu wakitengewa vituo saba.