February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

LISSU ASHIRIKI MKUTANO WA UCHAGUZI BOTSWANA, AKUTANA NA VIGOGO

Aliyekuwa Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Antipas Lisu leo Jumatatu Novemba 8, 2021 ameshiriki kwenye mkutano wa Kimataifa kuhusu chaguzi za Afrika unaoendelea Gaborone, Nchini Botswana.

Akiambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu ambaye alisimama kama mgombea mwenza wa Lisu wakati akiwania kiti cha Urais kupitia CHADEMA kwenye uchaguzi Mkuu 2020, Lisu amekutana na kuzungumza kwa kifupi na Balozi wa Ujerumani Nchini Botswana, Margit Hellwig-Boette.

Ikumbukwe siku chache baada ya uchaguzi mkuu Tundu Lisu alielekea Nchini Ubeligiji huku akieleza kuwa yupo nchini humo kwa sababu za kiusalama, huku akiomba mara kwa mara kuhakikishiwa usalama wake ili aweze kurejea nchini.

Hata hivyo Jeshi la Polisi Nchini Tanzania kupitia IGP, Simon Sirro limekuwa likisema Nchi ina usalama na kuhusu madai ya kushambiliwa kwake kwa risasi na madai ya kutofanyika kwa uchunguzi kwenye shambulio linalodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana, Kamanda Sirro ameeleza kuwa Jeshi la Polisi hufuata misingi taratibu kwenye uchaguzi hivyo milango ya uchunguzi ipo wazi iwapo Lissu atakuwa tayari kutoa ushirikiano.

Mnamo Agosti 2017 Tundu Lissu alishambiliwa kwa risasi zaidi ya 16 na watu wasiojulikana karibu na eneo la makazi ya Wabunge risasi zilizompelekea kuwa Nchini Ubeligiji kwa ajili ya matibabu, hata hivyo baada ya afya yake kuimarika alipitishwa na chama chake kuwania Urais wa Tanzania kupitia chama cha CHADEMA ndipo ilipombidi kurejea tena nchini Tanzania kushiriki uchaguzi na baada ya zoezi la uchaguzi kwisha alirejea tena nchini Ubelgiji alipohamishia makazi yake yapo kwa sasa.