Kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili kukusanya mapendekezo juu ya uboreshwaji demokrasia ya vyama vingi nchini, kinaendelea kupokea maoni ya wadau ambapo kwa sasa ni zamu ya vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo Jumamosi na Katibu wa Kikosi kazi hicho, Sisty Nyahoza, kuanzia tarehe 5 hadi 13 Mei, 2022, kitaanza kupokea maoni ya vyama vya siasa, kwenye ukumbi wa Adam Sapi Mkwawa, jijini Dar es Salaam.
“Tarehe 5 hadi 13 Mei, 2022, kikosi kazi kitaendelea kuongea na wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kupokea maoni na mapendekezo yao. Mazungumzo hayo yatafanyika katika Ukumbi wa Adam Sapi Mkwawa, wa ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam,” imesema taarifa ya Nyahoza.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Nyahoza, zoezi hilo litaanza tarehe 5 Aprili 2022, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT-Wazalendo na UMD, vitafungua dimba, huku Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi, vitawasilisha maoni yao tarehe 6 Mei mwaka huu.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ADC na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), vinatarajia kuwasilisha maoni hayo tarehe 9 Mei mwaka huu.
Vyama vingine vitaendeleakuwasilisha maoni yao, hadi itakapofika tarehe 13 Mei 2022.
Aidha, taarifa ya Nyahoza imesema, kikosi hicho kinakaribisha maoni ya wadau wengine, yatakayopokelewa kwa njia mbalimbali, ikiwemo barua pepe na barua nyaraka zitakazowasilishwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Taarifa hiyo imesema, maoni yanayopokelewa ni kuhusu mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, masuala yanayohusu uchaguzi, mfumo wa maridhiano ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Masuala mengine ni, ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi, elimu ya uraia, rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi, ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa, katiba mpya na uhusiano wa siasa na mawasiliano kwa umma.
Habari Zaidi
DCI KINGAI ASISITIZA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA KWA WATOTO WAO ILI KUPUNGUZA UKATILI
THRDC,C-SEMA YAENDESHA MAFUNZO KWA POLISI NA WAENDESHA MASHITAKA