March 23, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI YA PILI KUPINGA TOZO MIAMALA YA SIMU YATAJWA MAHAKAMA KUU.

Mwigulu Nchemba-Waziri wa Fedha na Mipango.

Na Leonard Mapuli

Kesi ya pili  iliyofunguliwa na Mwanaharakati wa Haki za Binadamu Charles Odero,kupinga uhalali wa ongezeko la tozo katika miamala ya fedha kwa njia simu,imetajwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama kuu Masjala Kuu ya Dar es Salaam leo,Agosti 12.

Katika kesi hiyo namba 14 ya mwaka 2021,dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango,pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,mwanaharakati huyo amedai kuathiriwa moja kwa moja na tozo hizo,zilizopitishwa na Bunge,baada ya wizara ya Fedha na Mipango kupendekeza ongezeko hilo la tozo kama njia mpya ya kuongeza mapato katika utekelezaji wa bajeti,kwa mwaka wa fedha 2021/22 na kuanza kutumika tangu Julai Mosi 20121.

Dar es Salaam, Tanzania – 2015-02-09 – Money illustrations in Dar es Salaam, Tanzania on February 9, 2015. Photo by Daniel Hayduk

Katika kesi hiyo,ambayo Mwanaharakati Odero amewasilishwa Mahakamani hapo na Wakili John seka,Mahakama imeipa Serikali muda wa hadi tarehe 17 mwezi huu (Julai)kufanya marejeo na itasikilizwa tena Agosti 18 chini ya Jaji John Samwel Mgeta.

Kesi hii imeanza kusikilizwa katika siku ambayo  mlalamikaji Charles Odero akitakiwa kuripoti katika ofisi za Uhamiaji mkoani Arusha,baada ya kupokea wito wa kumhitaji kufika katika ofisi hizo kwa mahojiano juu ya uraia wake,siku moja kabla ya kusikilizwa kwa kesi aliyoifungua.

Kesi hii ya kupinga uhalali wa ongezeko la tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya Simu, ni ya pili kutajwa mahakamani hapo ndani ya siku 17.Kesi ya kwanza ilifunguliwa Julai 27 na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC)na kutajwa kwa mara ya kwanza Agosti 5,na itasikilizwa kwa Mara ya pili Agosti 16 chini ya Jaji yule yule,John Mgeta.