February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI YA MBOWE YASOMWA MAELEZO YA AWALI, AGOMA KUTOA MAELEZO POLISI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeihamishia Kesi ya uhujumu uchumi namba 63/2021 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Denokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Freeman Mbowe na wenzake watatu katika Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi baada ya mahakama hiyo kusikiliza ushahidi na maelezo ya awali ya mashitaka (committal proceedings)  yanayowakabili watuhumiwa hao hii leo baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Kuwasilisha taarifa hizo Mahakama Kuu.

Akisoma maelezo hayo yaliyochukua takribani masaa manne mbele ya Hakimu Thomas Simba Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Kabuga amewasomea watuhumiwa mashitaka sita ikiwemo kula njama za kutenda kosa la ugaidi,kusababisha majeraha kwa aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya.

Pia Mbowe anashitakiwa kutoa kiasi cha shilingi laki sita za kitanzania kwa ajili ya kufadhili matendo ya ugaidi,na katika kosa lingine watuhumiwa wote wanashitakiwa kwa kushiriki vikao vya kutenda ugaidi,Mtuhumiwa wa pili anashitakiwa kwa kumiliki bastola yenye risasi tatu kwa ajili ya kutenda makosa ya kigaidi na mshitakiwa mwingine anatuhumiwa kumiliki nguo za Jeshi la Wananchi Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa.

Upande wa mashitaka umesema unatarajia kutumia mashahidi 24 na vielelezo vya maandishi 19 na miongoni mwa mashahidi watakaowatumia katiak kesi hiyio  ni wanasheria wa Kampuni ya Tigo  na Airtel waliotoa taarifa za miamala kutoka kwa Freeman Mbowe kwenda kwa washitakiwa wenzake.

Katika shauri hilo mshitakiwa namba nne, Freeman Mbowe amekataa kutoa maelezo yake kwa polisi na kueleza kuwa atatoa maelezo yake mahakama Kuu, hata hivyo washitakiwa wengine wameieleza mahakama kuwa maelezo yaliyosomwa katika hati ya mashitaka yanayodaiwa ni ya kwao waliyatoa bila hiyari baada ya kupigwa na kulazimishwa kusaini maelezo hayo.

Aidha upande wa Utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala umeieleza mahakama kuwa wanatarajia kuwaita Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya kama mashahidi wao wa upande wa utetezi na kuongeza kuwa wataendelea kuleta mashahidi wengine wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa.

Kabla na baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kulikuwa na hali ya utulivu mahakamani hapo na  ulinzi uliimarishwa na kila aliyeingia katika viunga vaya mahakama hiyo alipaswa kukaguliwa.