February 3, 2023

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI YA MBOWE NA WENZAKE YALINDIMA, PINGAMIZI LAO LAKUBALIWA

Na: Anthony Rwekaza

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Jumatatu Januari 10, 2022 imekubali pingamizi lililowekwa na Mawakili wa upande wa utetezi, wakipinga ombi la kupokelewa kwa sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutopokelewa na Mahakama kama moja ya kielelezo kutoka upande wa Jamhuri.

Ikumbukwe Kesi hiyo aamba 16/ 2021 yenye mashtaka ya Ugaidi inawakabili washtakiwa wanne akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ambaye ni mshtakiwa namba nne, Kesi hiyo iliharishwa kupisha mapumziko ya sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya ambapo ilikuwa inasikilizwa mfululizo na Jaji Joachim Tiganga.

Awali katika pingamizi hilo upande wa utetezi uliiomba Mahakama kutokipokea kielelezo hicho, huku wakiwatoa hoja kuwa hakikufuata utaratibu wa ukamataji mali wakati ambapo upande wa Jamhuri ukiiomba Mahakama hiyo kupokea sare hizo zilizodaiwa kukutwa na Halfani Bwire Hassan ambaye ni mshtakiwa namba moja kwenye kesi hiyo ili zitambuliwe kuwa kielelezo cha ushahidi wake.

Katika Kesi hiyo ambayo upande wa Jamhuri unaendelea kutoa ushahidi, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka tofauti ikiwemo kudaiwa kupanga njama za kutenda ugaidi ikiwemo kulipua vituo vya mafuta, huku Mbowe kwenye mashtaka hayo anadaiwa kufadhili Ugaidi kiasi cha Shilingi laki sita.