December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI YA MBOWE NA WENZAKE YAKWAMISHWA NA MTANDAO,KUSIKILIZWA TENA AGOSTI 6

Na Leonard Mapuli

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeshindwa kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) baada ya kukosekana kwa mawasiliano Madhubuti ya kimtandao,baina ya Mahakama hiyo na Gereza la Ukonga aliko mwenyekiti huyo na wenzake watatu.

Kwa mujibu wa maelezo ya awali yaliyowasilishwa na Mahakama,Kesi hiyo ilishindwa kusikilizwa kwa njia ya kawaida (Mbowe na wenzake kufika Mahakamani) kwa  sababu za hofu ya janga la Uviko-19 ambapo mahakama hiyo iliamua kuisikiliza kesi hiyo kwa njia ya Video Mtandao (Video Conference).

Mawakili wanaomtetea Mbowe wakiongozwa na Peter Kibatala Pamoja na baadhi ya viongozi wa Chadema wakiongozwa na Katibu Mkuu John Mnyika,walifika Mahakamani hapo mapema na kuingia kwenye chumba cha kusikiliza kesi hiyo iliyokwamishwa na mawasiliano duni ya imtandao.

“Leo ndiyo siku iliyokuwa imepangwa kwa mwendelezo wa hatua za kisheria kusikiliza shauri husika,na tulitegemea kwamba kama kawaida (Mbowe) ataletwa mahakamani pamoja na washtakiwa wenzake,lakina kwa sababu moja ama nyingine,leo hawakuweza kufika ambapo wenzetu  (Mahakama)wametoa sababu ikiwemo Corona”,ameeleza Wakili Peter Kibatala alipozungumza na wandishi wa Habari waliofurika kwa wingi mahakamani hapo kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.

Baada ya kushindwa kusikilizwa kwa kesi hiyo leo,mahakama imetoa maelekezo kuwa washtakiwa wote watafikishwa Mahakamani hapo kesho (August 6) majira ya tatu asubuhi,na mambo yote ya kisheria yaliyopangwa kufanyika leo yatafanyika siku ya kesho .

Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika na baadhi ya wanachama wakiondoka mahakamani Kisutu.

Katika hali ya sintofahamu,wakati juhudi za mawasiliano baina ya mahakama ya Kisutu na gereza la Ukonga zikiendelea ndani ya ukumbi wa mahakama,askari polisi waliovalia sare za jeshi hilo na wengine kiraia waliwazingira wanaooaminika kuwa ni wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika nje kabisa ya lango kuu na ngome ya mahakama hiyo,wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali zote za kuiomba serikali na Mahakama,kumuachia huru Freeman Mbowe.Aidha baada ya kuwazingira,walikamatwa na kupigwa “Tanganyika jeki” kisha kupandishwa kwenye gari la polisi lililokuwa na askari waliojihami kwa silaha za moto.

Hata baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo,askari polisi walitanda katika lango kuu la Mahakama hiyo ambapo pia walikamata watu kadhaa waliokuwa na mabango,moja likisomeka “Mbowe sio Gaidi”,ambao pia walipandishwa kwenye gari la polisi.

“Kamanda,siyo kosa mtu kushikilia bango nje ya Mahakama,mnachokifanya ni kinyume cha sheria”,amesikika wakili Peter Kibatala ,akizungumza huku akisogelea gari la polisi walimokuwa wamepakiwa watu hao baada ya kukamtwa.

Freemani Mbowe na wenzake,wanakabiliwa na makosa mawili ya jinai,ikiwemo kupanga njama za kulipua vituo vya mafuta,Pamoja na mikusanyiko  kinyume na vifungu  namba 4 (1),3 (i),na 27 (c) vya sheria namba 21 ya mwaka 2002 ya kuzuia ugaidi.Katika Shtaka jingine,watuhumiwa wanakabiliwa na kesi ya kufadhili ugaidi,kinyume na sheria ya kuzuia ugaidi yam mwaka 2002.

Mbowe na wenzake,wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya tarehe 1 mei,na tarehe 1 Agosti mwaka 2020 katika miji ya Moshi,Arusha,Morogoro,na Dar es Salaam.

Hata hivyo,wafuatiliaji na wachambuzi wa masuala ya kisiasa nje na ndani ya Tanzania wanaihusisha kesi hiyo kama “Maji” ya kuuzima mjadala wa katiba mpya ,ambao hadi kukamatwa kwake,Mbowe alikuwa katika maandalizi ya Kongamano kubwa la Katiba mpya jijini Mwanza ambako yeye na viongozi wengine wa chama hicho,walikamatwa usiku,siku moja kabla ya kongamano hilo.