December 4, 2022

Watetezi Media

Official Website for Watetezi Media

KESI YA MBOWE NA WENZAKE: MAHITA ASIMULIA WALIVYOWATIA NGUVUNI MAKOMANDO

Aliekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Arusha mjini, Inspecta Omari Mahita ameiambia Mahakama kuwa alipigiwa simu na aliyekuwa RCO Arusha mjini, ACP Ramadhani Kingai tarehe 04/08/2020 akimtaka aende ofisini kwake ili ampe maelekezo ya kazi kuwa kuna watu walikuwa wanapanga njama za kufanya ugaidi pamoja na kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na kwenda kuwakamata kabla hawajatekeleza vitendo hivyo

Omari Mahita ni shahidi wa pili upande wa Jamhuri katika shauri dogo la kesi mama Inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake watatu na anatoa ushahidi huo kuithibitishia mahakama kuwa mshitakiwa wa pili Adam Hassan Kusekwa hakuteswa kabla na wakati akichukuliwa maelezo ya onyo katika pingamizi lililowekwa na upande wa utetezi.

Akiongozwa na Wakili wa serikali Mwandamizi, Pius Hilla shahidi ameieleza mahakama kuwa walipata taarifa kuwa watuhumiwa wapo Moshi mjini na walifika siku hiyo ili kuwakamata lakini taarifa hazikukaa vizuri hivyo hawakufanikiwa kuwakamata watuhumiwa kwa siku hiyo.

“ilivyofika usiku wa saa tano au sita tukapumzika ili tuendelee na upelelezi siku inayofuata,”amesema.

Shahidi huyo ameeleza kuwa ilipofika majira ya saa sita mchana siku ya tarehe 5/08/2020, ACP kingai aliwaeleza kuwa watuhumiwa wameonekana eneo la Rau madukani na kwakuwa wanakwenda kufanya kazi ya ukamataji wakamwuliza kuhusu mwonekano wao na walielezwa namna watuhumiwa walivyovalia.

Amesema baada ya kufika eneo la tukio walifanya ‘surveillance’ na wakagundua watuhumiwa walikuwa kwenye banda la supu, hivyo wakashusha kikundi cha kwanza upande wa kulia na section ya pili akiwa yeye (Mahita) na wengine upande wa kushoto na gari ikaenda mbele kidogo.

Akiendelea kutoa ushahidi wake ameeleza mahakama kuwa waliwagundua watuhumiwa kutokana na mavazi na kuwaamuru wasimame kwa kuwa wapo chini ya ulinzi na walitii wakakaa chini na kuweka mikono juu, baada ya hapo alijitambulisha na kuwaonya watuhumiwa kwa kosa walilokuwa wakituhumiwa nalo la kula njama za kutenda vitendo vya ugaidi.

Mahita amesema kwa kuwa timu aliyokuwa nayo haikuwa mbali walifika na kuimarisha ulinzi na baada ya ACP Kingai kufika alimpa maelekezo ya oda kwa Afande Jumanne kuwapekua watuhumiwa ambapo baada ya upekuzi mtuhumiwa Adam Kasekwa alikutwa na Pistol yenye risasi tatu upande wake wa kushoto na kete 58 za madawa yanayosadikiwa kuwa ya kulevya, na mtuhumiwa Mohamed Ling’wenya alikutwa na kete 25 za madawa hayo.

Shahidi ameendelea kusema Afisa Mpekuzi alijaza hati ya upekuzi ambayo ilisainiwa na watuhumiwa na mashahidi huru aliowataja kwa jina la Anitha na Ester kisha watuhumiwa na mashahidi huru wakachukuliwa hadi Kituo cha Polisi Kati mjini Moshi ambapo mashahidi hao waliandikishwa maelezo.

Mahita ameiambia mahakama kuwa wakati wakielekea kituoni, ACP Kingai aliwauliza watuhumiwa kuwa walikuwa watatu na mtuhumiwa Moses Lijenje yupo wapi ambapo watuhumiw hao walimjibu kuwa walikuwa naye eneo la Rau madukani na wakakubali kuonyesha alipo

“ilipofika asubuhi saa 11-12 tuliwafuata watuhumiwa na kuwatoa mahabusu tukaenda stendi kuu na watuhumiwa,askari wengine wanazunguka maeneo mbalimbali tulikaa pale hadi saa tatu mpaka nne bila mafanikio.kwa vile tulikuwa tumeamka mapema tulikunywa chai tuakendelea na upelelezi,”ameiambia mahakama.

Shahidi huyo ameendelea kuieleza mahakama kuwa mnamo tarehe 6/08/2020, ACP Kingai aliwapa maelekezo ya kuanza safari ya kuelekea Dar es salaam ambako kesi ilikuwa imefunguliwa lakini wakiwa njia panda ya Himo gari ilipata pancha na wakati wanasubiri gari ingine walipata chakula cha usiku pamoja na watuhumiwa na walifika Dar es salaam alfajiri.

Amesema tarehe 08/08/2020 ACP Kingai alielekeza watuhumiwa watolewe Kituo cha Polisi Kati Dar es salaam na kuwapeleka kituo cha Mbweni kutokana na mafunzo ya kikomando waliyopitia watuhumiwa hivyo wanahitaji kuwepo eneo ambalo halina mwingiliano wa watu wengi na walihitaji kuwekwa mahabusu tofauti ili ushahidi usivurugike.Mahita ameiambia mahakama kuwa watuhumiwa hawajateswa tangu walipokamatwa na waliwatendea kwa utu na heshima kama binadamu wengine.

Akihojiwa na Wakili wa mshitakiwa wa nne, Peter Kibatala kama taarifa za yeye kufika mahakamani kutoa ushahidi Mahita alieleza mahakama kuwa alipata taarifa hizo hapo jana kutoka kwa shahidi namba moja ACP, Kingai kuwa anatakiwa kutoa ushahidi wake hii leo.

Kutokana na muda Wakili Peter Kibatala aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Jumatatu ambapo Wakili huyo ataendelea kumhoji Shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri, baada ya kusikiliza pande zote Jaji Mustapha Siyani aliahirisha shauri hilo dogo hadi tarehe 20/09/2021 saa nne kamili asubuhi ili kuendelea na maswali ambayo Wakili wa mshitakiwa wanne atamalizia kumhoji shahidi na upande wa Jamhuri kumalizia kumhoji shahidi wao.